Maelfu ya watu wameuawa tangu vita nchini Sudan vilipoanza katikati ya Aprili 2023. / Picha: AFP

Jeshi la Sudan limetangaza kuwa limepata tena udhibiti wa Al-Hasaheisa na Al-Rufaa katika Jimbo la Al-Jazira kutoka mikononi mwa Vikosi vya RSF.

"Leo, vikosi vyetu, pamoja na Vikosi vya Ngao ya Sudan vinavyoongozwa na Abu Aqla Keikel, vimefanikiwa kukomboa miji ya Al-Rufaa na Al-Hasaheisa," kamanda wa uwanja Kanali Al-Abadi Al-Tahir alisema katika video iliyowekwa na jeshi, kwenye Facebook siku ya Jumamosi.

Jeshi lilisema katika taarifa yake kwamba "vikosi vya jeshi na Vikosi vya Ngao ya Sudan, chini ya uongozi wa Abu Aqla Keikel, vinapiga hatua katika maeneo ya Al-Hasaheisa na Al-Rufaa, na kuwasababishia hasara kubwa wanamgambo wa RSF, pamoja na kuwakabili wale wanaokimbia."

Mashambulizi hayo yametoa fursa kwa jeshi kudhibiti Al-Hasaheisa, mji wa pili kwa ukubwa katika Jimbo la Al-Jazira, lililoko kilomita 55 kutoka Wad Madani, mji mkuu wa jimbo hilo, pamoja na Al-Rufaa, mji mkubwa zaidi wa jimbo la mashariki la Al-Jazira.

Jeshi lachukua tena udhibiti wa Wad Madani

Jeshi lilitangaza Januari 11 kuingia kwake Wad Madani, karibu mwaka mmoja baada ya kupoteza udhibiti wa jiji hilo kwa RSF.

Baadaye, kamanda wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kwa jina la Hemedti, alikiri kupitia sauti iliyorekodiwa kwamba vikosi vyake vimeshindwa kudhibiti mji wa Wad Madani.

TRT Afrika