Nchi zinazozalisha pamba kwa wingi barani Afrika, zimelitaka Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO) kutafuta suluhisho la upotoshaji wa biashara hiyo, unaofanywa na nchi hizo zilizoendelea.
Wito huo unakuja kabla ya kikao cha mawaziri wa WTO kinachofanyika katika mji wa Abu Dhabi, siku ya Jumatatu.
Nchi hizo, maarufu kama C4, zinazohusisha Benin, Burkina Faso, Mali na Chad, zimetaka kuondolewa kwa ruzuku ya bei ya pamba kwa nchi za Marekani, India na China, zikidai zinaathiri bei ya ndani ya bidhaa hiyo.
"Hali hii imeathiri biashara ya pamba kwa miaka 20 na kuathiri maisha ya mamilioni ya watu barani Afrika," amesema Ahmat Abdelkerim, Waziri wa Viwanda na Biadhara wa Chad, katika mkutano na wanahabari kwa niaba ya nchi za C4.
'Mchango mkubwa'
C4 pia ilitoa wito wa kulipwa fidia kwa uharibifu uliosababishwa hadi sasa, na suala la pamba kuondolewa kwenye ripoti ya kilimo ili kuendeleza majadiliano.
Ivory Coast na nchi nyengine za C4 zimewasilisha rasimu ya maamuzi ya suala hilo kwa WTO, kama maandalizi ya mkutano unaofanyika Umoja wa Falme za Kiarabu siku ya Jumatatu.
Hata hivyo, Waziri huyo wa Chad alisema rasimu ya uamuzi huu "haujazingatiwa" ingawa pamba ni muhimu "sio tu kwa ajili ya kutengeneza ajira, bali pia kwa usalama wa chakula."
"Itachangia kwa kiasi kikubwa kwa amani ya bara la Afrika," aliongeza.
Sekta ya pamba inaajiri zaidi ya watu milioni 20 katika nchi za C4, ikiwa na thamani ya dola bilioni 2, kulingana na Ibrahim Malloum, mwakilishi wa Chad anayehusika na masuala ya biashara.
Minyororo ya thamani
"Suala ni la usawa na haki ya kiuchumi," aliongeza Waziri wa Viwanda na Biashara wa Mali, Moussa Alassane Diallo, katika mkutano huo wa waandishi wa habari.
Mkurugenzi Mtendaji wa WTO, Ngozi Okonjo-Iweala na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino, siku ya Jumamosi walisema kuwa taasisi hizo mbili wataimarisha ushirikiano wao kwenye maendeleo ya zao hilo na kutoa wito wa umuhimu wa kuhusisha nchi za Afrika katika minyonyoro ya thamani ya pamba.
Suala la kilimo halina uwezekano wa kupiga hatua katika mkutano wa WTO huku mataifa kadhaa yakipinga vikali hatua zilizopendekezwa kwa kuhofia zitatatiza masoko ya chakula duniani.