Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) kimeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali mbaya kwa watu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo), hasa katika jimbo la Kivu Kusini.
“Ikiwa hali ya usalama nchini DRC haitatatuliwa, pamoja na kusimamishwa kwa ufadhili wa Marekani, basi tunacheza na moto,'' Mkurugenzi Mkuu Jean Kaseya alisema katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari za mtandaoni siku ya Alhamisi.
''Tumeona DRC ikiwa kitovu cha mlipuko mkubwa wa janga ambalo linaweza kuenea zaidi hadi nchi nyengine katika eneo hilo. Nimewaandikia wakuu wote wa nchi katika bara nikiomba kuungwa mkono ili kutuwezesha kutoa misaada kwa watu wa Kivu Kusini,” Kaseya aliongeza.
Zaidi ya watu milioni 7 wamekimbia makazi yao nchini DRC kutokana na mzozo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 20, kwa mujibu wa Rais wa DRC.
Mawasiliano na Dangote
Waasi wa M23 waliiteka Goma na baadaye kusonga mbele hadi Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini. Kaseya alisema mazungumzo na Marekani yanaendelea ili kufanikisha msaada ulioahidiwa wa dola milioni 385, kutoka dola milioni 500 kabla ya kusitishwa kwa msaada huo.
"Tulipokea dola milioni 4 kutoka China na Korea Kusini, lakini hizi hazitoshi ikilinganishwa na kiwango kilichoahidiwa na Marekani," Kaseya alisema.
Alisema kando ya mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Februari 15 na 16, mjini Addis Ababa, Ethiopia, alimshirikisha bilionea wa Afrika, Aliko Dangote na mhisani Tony Elumelu ili kuunga mkono mpango mpya wa ufadhili unaoanzishwa na kamati ya Afrika CDC.
Chanjo zaidi
"Pia tunalenga kuhakikisha kuwa Afrika inaanza kutengeneza chanjo yake ya kipindupindu mwaka 2025. Kwa chanjo ya Mpox, katika siku chache zijazo tutakuwa tukikamilisha mazungumzo yanayoendelea na Bavarian Nordic," aliongeza.
Tangu Januari 26, mzozo nchini DRC umesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000, takriban majeruhi 3,000, na zaidi ya watu nusu milioni waliohama makazi yao. Pia kuna watu milioni 6.4 ambao tayari wamekimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Takriban wanajeshi 20 wa kulinda amani wakiwemo 14 wa Afrika Kusini wameuawa katika mapigano kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa DRC. Kinshasa imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 na kupeleka wanajeshi mashariki mwa DRC kuwasaidia waasi hao katika mashambulizi yao ya hivi majuzi. Hata hivyo, Kigali imekanusha mara kwa mara madai haya.