Marais wa Afrika Mashariki walifanya mkutano mtandaoni kujadili mzozo nchini DRC. /Picha:  Rais Yoweri Museveni 

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imemtaka Rais Felix Tshisekedi kufanya mazungumzo na wadau wote katika mzozo wa mashariki mwa DRC, wakiwemo Rwanda na kundi la waasi la M23.

Hali ni ya taharuki katika eneo la Goma mashariki mwa DRC ambapo waasi wa M23 wameripotiwa kudhibiti eneo hilo.

Siku ya Jumatano, Januari 29, wakuu wa nchi za EAC wamefanya mkutano maalum wa viongozi kuhusu mzozo unaozidi kuongezeka mashariki mwa DRC.

Rais William Ruto, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya EAC ameongoza mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao.

Kando na Rais Ruto, mkutano huo ulihudhuriwa na marais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia na Evariste Ndayishimiye wa Burundi.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi, ambaye nchi yake ni sehemu ya Jumuiya ya EAC, hakuhudhuria mkutano huo licha ya Rais Ruto kuthibitisha mapema wiki hii kwamba kiongozi huyo wa DRC atahudhuria.

"Mkutano huo ulitoa wito wa kusuluhishwa kwa amani migogoro hiyo na kuitaka serikali ya DRC kuwasiliana moja kwa moja na wadau wote, ikiwa ni pamoja na M23 na makundi mengine yenye silaha ambayo yana manung'uniko," kulingana na taarifa iliyotolewa baada ya mkutano.

"Mkutano huo ulitoa wito kwa pande zote katika mzozo wa mashariki mwa DRC kusitisha uhasama na kuzingatia usitishaji mapigano mara moja na bila masharti na kuwezesha upatikanaji wa misaada kwa watu walioathirika," iliongezea.

Rwanda imekataa shutuma za DRC, Umoja wa Mataifa na Marekani kuwa inaunga mkono waasi wa DRC.

Mkutano mwingine wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wale wa Jumuiya ya Afrika Kusini ( SADC) ambapo DRC pia ni mwanachama unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

TRT Afrika