Serikali imetangaza kufungwa kwa shule zote kwa muda wa wiki mbili kutokana na joto kali linaloendelea ambalo inasema limesababisha baadhi ya wanafunzi kuanguka.
Hii ni mara ya pili kwa nchi hiyo - ambayo inakabiliwa na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa, pamoja na mafuriko wakati wa msimu wa mvua - kufunga shule wakati wa kipindi cha joto kali mnamo Februari na Machi mwaka 2024.
Machi 2024, shule nchini humo zilifungwa kwa wiki mbili kufuatia joto lililofikia nyuzi joto 45.
Naibu Waziri wa Elimu Martin Tako Moi alisema Alhamisi "takriban wanafunzi 12 wamekuwa wakianguka katika jiji la Juba kila siku."
Shule nyingi nchini humo zimejengwa kwa mabati na hazina umeme unaoweza kuwasha viyoyozi.
Waziri wa Mazingira Josephine Napwon Cosmos nae aliwataka wakaazi kubakia majumbani na kunywa maji kwa wingi kutokana na hali hiyo ya kupanda kwa nyuzi joto.
"Joto hatari kama hili ni tatizo kwa afya ya mwili na akili ya watoto. Kwa sababu miili yao bado inakuwa, wako hatarini zaidi kwa magonjwa ya haraka na madhara ya muda mrefu ambayo huja na usumbufu mkubwa, kukosa usingizi na uchovu," amesema Christopher Nyamandi, Mkurugenzi wa Shirika la Save the Children nchini Sudan Kusini.
Shirika hili linasema kuwa shule kufungwa kwa sababu ya joto kali imechangia watoto wengi kukosa masomo hivyo kuwaingiza katika hatari ya ndoa za utotoni, ajira za watoto na kuingizwa katika vikundi vyenye silaha.