Xi Jinping kuongoza China kwa muhula mwingine wa tatu

Rais Xi Jinping amejishindia muhula wa tatu kuendelea kuiongoza China na kumfanya kuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa zaidi nchini humo tangu enzi za mwanzilishi Mao Zedong.

Kwa mujibu wa kituo cha Serikali ya China, Kamati Kuu ya Chama cha Komunisti ilimchagua Xi kuendelea kuongoza kwa muhula mwingine wa miaka mitano. Wamuzi huo unakuja baada ya mchakato mpana uliodumu kwa wiki moja jijini Beijing, ambapo Wakuu wengine wa chama hicho walidadisi kwa makini anayepaswa kumrithi Xi lakini ikabainika wazi kuwa ni busara zaidi Xi aendelee kuongoza.

Ni wazi sasa kuwa Xi Jinping ataendelea kuwa Rais na tangazo rasmi juu ya muhula wa tatu litafanyika mwezi Machi mwaka 2023. Aidha chama cha Komunisti kilichagua kamati kuu mpya inayosadikiwa kuwa na viongozi wakuu wapatao 200; mkubwa zaidi akiwa ni Xi Jinping.

Tangu achaguliwe kuwa Rais miaka 10 iliyopita, Xi amefanikiwa kujipatia mamlaka kubwa zaidi kuliko kiongozi mwengine yeyote katika historia ya China isipokuwa mwanzilishi Mao.

Ikumbukwe pia Xi alifutilia mbali sheria ya kuongoza kwa mihula miwili tu mwaka wa 2018; jambo lililotafsiriwa na wengi kama njama ya kutaka kudumu uongozini kwa muda usiojulikana.

Aidha Rais Xi amefanikiwa kukuza uchumi wa China na kuufanya wa pili kwa ukubwa duniani pamoja na kuleta maendeleo makubwa katika nguvu silaha ya Jeshi la nchi hiyo, jambo ambalo limeonekana kuikera Marekani.

Hatahivyo Kiongozi huyo anakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile; chuki na uhasama kutoka kwa taifa la Marekani.

AFP