Watu wanaodaiwa kuwa mamluki wa Nazi wateketeza kituo cha wakimbizi nchini Ujerumani

Kituo cha wakimbizi kutoka Ukraine kilichoko kaskazini mwa Ujerumani kiliteketezwa moto Jumatano usiku na watu wasiojulikana, vyanzo vya habari nchini Ujerumani vimeripoti.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, hakuna aliyejeruhiwa kati ya wakimbizi hao 14 waliokuwa wakiishi pamoja kwenye kituo hicho ambacho zamani kilikuwa ni mgahawa, katika mji mdogo wa Gross Stromkendorf jimbo la Mecklenburg-Western Pomerania.

Grafiti ya Swastika

Kwa mujibu wa ripoti ya awali kutoka kwa vituo vya habari nchini Ujerumani, maafisa wa polisi walizuru kituo hicho wikiendi iliyopita baada ya kuonekana kwa graffiti ya swastika ikiwa imechorwa juu ya kibao cha kuonesha kiingilio.

Tino Schomann, ambaye ni afisa wa Wilaya aliambia wanahabari: “Kwa uzoefu wangu kwenye zima-moto, nadhani moto huu ulianzishwa maksudi.”

Kwa mujibu wa kitengo cha zima-moto hawakuwa na budi ila kusubiri jengo kuteketea taratibu kwani wasingeweza kuokoa chochote.

Wakimbizi hao walihamishiwa sehemu nyingine na mamlaka za Wilaya.

Eneo la tukio ni karibu na eneo ambapo mwaka 1992 kulishuhudiwa vurugu kutoka kwa mamia ya watu wakipinga hatua ya serikali ya Ujerumani kuwapa hifadhi wahamiaji kutoka nchi nyingine.

Vurugu hizo zilipelekea pia kuteketezwa moto nyumba moja ya raia wa Turkiye na mamluki wa Nazi.

Reuters