Haijakuwa muda mrefu tangu Monique Ruck mwenye umri wa miaka 34 na mama wa watoto watatu, kuanza kwenda kwenye kituo cha burudani karibu na nyumbani kwake mashariki mwa Mji mkuu wa Berlin. Kituo hicho kinaendeshwa na Die Arche, ambalo ni shirika la utoaji msaada kwa ajili ya watoto.
Monique ambaye analea watoto wake pekee yake amekuwa akizuru kituo hicho na binti yake mdogo ambapo wamekuwa wakipata nafasi ya kucheza na walau kupata chakula kidogo cha kutia mdomoni na kubebea wanawe wengine wawili. Aidha Die Arche pia husaidia wazazi na vifaa kadha wa kadha vya kusomea kwa ajili ya watoto wao.
Hatua hii imembidi kuchukua kutokana na hali ngumu ya maisha ikiwemo ongezeko la bei ya gesi linalokumba Ujerumani sasa hivi. Bei za nishati zimeongezeka pakubwa nchini humo kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Ujerumani inategemea pakubwa gesi kutoka Urusi.
Akizungumza na TRT World wakati bintiye akicheza pembeni, Monique anasema hali ni ngumu sana kwa familia yake.
“Sio tu bei za nishati zimepanda lakini hata chakula na mafuta ni ghali kununua.” Anasema Monique.
“Nahitaji kutumia gari kila siku kuwapeleka shule wanangu lakini sijui nitafanyaje ikitokea gari langu limeharibika. Naogopa mambo huenda yakawa mabaya hata zaidi katika siku zijazo. Najua siko pekee yangu kwenye tatizo ila kwa kweli naogopa.” Anaeleza zaidi.
Msemaji wa shirika la Die Arche Wolfgang Buescher anasema kuwa wanatoa msaada kwa zaidi ya familia 5,000 katika maeneo tofauti nchini Ujerumani na familia takriban 1,800 katika Mji wa Berlin. Asilimia 95 ya familia hizo zina mzazi mmoja pekee, ambaye ni mama tu na wanae.
“Sasa hivi tuna wazazi wanaokiri kuwa hawana chakula cha kutosha nyumbani na inawabidi watoto wao kutokula chochote mchana kusudi jioni wasikose cha kutia mdomoni,” anasema Wolfgang.
Aidha anaongeza kuwa huenda hali ikawa mbaya hata zaidi ikizingatiwa kuwa watu wenye uhitaji wanaongezeka kila siku.
“Inawezekana idadi ya familia zenye uhitaji ikaongezeka hasa zilizowasili kutoka Ukraine na Uarabuni hapo miaka ya nyuma.”
Abi Saripalli ambaye mhandisi wa data kutoka India amekuwa akiishi Berlin kwa takriban miaka 10, na anasema imembidi yeye na mumewe kuwa makini na jinsi wanavyoishi kwani kuna hofu bei ya gesi na bidhaa nyengine ikaongezeka maradufu.
“Tunalipa zaidi ya euro 90 kila mwezi kupata umeme na tumeelezwa kuwa kiasi hicho huenda kikaongezeka maradufu hivi karibuni. Tumepunguza matumizi yetu ya umeme nyumbani. Tumenunua hata nguo za kujistiri wakati wa majira ya baridi badala ya kutumia umeme.” Anasema Abi.
Mwengine mwenye hofu ni Helga Roehle, ambaye ni meneja wa kituo cha kuogea cha kituruki kilichoko katika wilaya ya Kreuzberg.
“Kawaida tunatumia umeme mwingi kuongeza joto maeneo ya ‘sauna’ na ‘spa’ lakini sasa tumeelezwa kuwa huenda gharama ya umeme sasa tunaotumia sisi ikaongezeka mara sita,” anasema Helga na kuongeza kuwa hawana budi pia kuongeza gharama ya utoaji huduma kwa wateja wao.
“Kwa kweli hali halisi sio nzuri. Tumetoka tu kwenye kipindi kizito cha janga la corona na sasa vita vya Urusi na Ukraine vimeanza kutatiza, Sijui kesho itakuwaje.” Analalamika Helga.