Waandalizi wa Paris 2024 wamelazimika kuomba msamaha kwa maumini wa imani ya kikristu, hasa Katoliki na vikundi vingine vya Kikristo vilivyokasirishwa na muigizo wa sherehe ya pasaka. Wengi wamelalamika kuwa hiyo ilikuwa dhihaka kwa imani yao.
Hata hivyo waandalizi wa hafla hiyo wamejitokeza kuomba radhi kwa yeyote aliyechukizwa
Viongozi mbali mbali wa kidini pamoja na waumini wa kawaida mitandaoni wameelezea kuchukizwa na sehemu ya hafla hiyo ya ufunguzi wakiikashifu Ufaransa kwa kupoteza hadhi ya kidini na mila ya Ukristu.
Anne Descamps, msemaji wa Paris 2024 alisema katika taarifa Sherehe ya ufunguzi ilijaribu kusherehekea uvumilivu wa jamii.
"Ni wazi kwamba hakukuwa na nia ya kutoheshimu kikundi chochote cha kidini. (Sherehe ya ufunguzi) ilijaribu kusherehekea uvumilivu wa jamii,'' alisema Descamps katika taarifa kwa waandishi wa habari.
"Tunaamini azma hii ilifikiwa. Ikiwa watu wametenda kosa lolote tunasikitika sana." aliongeza.
Sehemu ya halfa hiyo y aufunguzi ilikuwa na sehemu ya maigizo iliyoanana na tukio la kibiblia la Yesu Kristo na wafuasi wake wakishiriki mlo wa mwisho au karamu ya bwana wakati mwingine ikiitwa Pasaka, kabla ya kusulubishwa na iligeuzwa kuonyesha malkia wa wapenzi wa jinsia moja akikokotwa, mwanamitindo aliyebadili jinsia na mwimbaji aliyekuwa uchi aliyeashiria mungu wa kishirikina wa Ugiriki aliyeitwa mungu wa divai Dionysus.
Ufaransa, ingawa inajivunia urithi wake tajiri wa Kikatoliki, pia ina mapokeo ya muda mrefu ya kutokuwa na dini na kupinga ukasisi. Kukufuru sio tu halali, bali pia inachukuliwa na wengi kama nguzo muhimu ya uhuru wa kusema.
Hata hivyo, kanisa katoliki nchini Ufaransa lilisema lilichukizwa na sherehe "iliyojumuisha matukio ya dhihaka na kejeli za Ukristo".