Raia wa Ufaransa waliokomaa kielimu haswa kutoka asili za Kiislamu, mara nyingi huwa ni watoto wa wahamiaji, wanaondoka Ufaransa, kutafuta mwanzo mpya nje ya nchi katika miji kama London, New York, Montreal au Dubai, kulingana na utafiti mpya.
Waandishi wa "Ufaransa, unaipenda lakini unaiacha," iliyochapishwa mwezi uliopita, walisema ilikuwa vigumu kukadiria ni wangapi haswa wameondoka.
Lakini waligundua kuwa asilimia 71 ya zaidi ya watu 1,000 waliojibu uchunguzi wao uliosambazwa mtandaoni, baadhi za sababu za kuondoka kwao ni ubaguzi wa rangi na kubaguliwa.
Adam, ambaye aliomba jina lake la ukoo lisitumike, aliiambia AFP kuwa kazi yake mpya katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu imempa mtazamo mpya.
Nchini Ufaransa "unahitaji kufanya kazi kwa bidii maradufu unapotoka tabaka la wachache," alisema.
Alisema "anashukuru sana" kwa elimu yake ya Kifaransa na amewakumbuka marafiki zake, familia na utajiri wa kitamaduni ya nchi aliyokulia.
Lakini alisema alifurahi kuachana na nchi yenye chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na "ubaguzi wa kimfumo" ambao ulimaanisha kuwa alisimamishwa na polisi bila sababu.
Ufaransa kwa muda mrefu imekuwa nchi ya wahamiaji, haswa kutoka makoloni yake ya zamani katika Afrika Kaskazini na Magharibi.
Lakini leo vizazi vya wahamiaji Waislamu waliokuja Ufaransa kutafuta mustakabali mwema wanasema wamekuwa wakiishi katika mazingira ya uhasama.
Wanasema mfumo wa Ufaransa wa kutokuwa na dini, ambayo inapiga marufuku alama zote za kidini katika shule za umma ikiwa ni pamoja na hijabu na majoho marefu, unaonekana kupiga vita kwa kiasi kikubwa mavazi ya wanawake wa Kiislamu.
Muislamu mwengine wa Ufaransa, mfanyakazi wa teknolojia mwenye umri wa miaka 33 mwenye asili ya Morocco, aliiambia AFP kuwa yeye na mke wake mjamzito walikuwa wakipanga kuhamia kwenye jamii yenye amani zaidi kusini mashariki mwa Asia.
Alielezea kutaka kuondoka kwenye "giza hili," ambapo vituo vya habari vya televisheni vinaonekana kuwalenga Waislamu wote kama mbuzi waliotolewa kafara.
Mfanyakazi huyo wa teknolojia, ambaye alihamia Paris baada ya kukulia katika vitongoji vya mapato ya chini, alisema amekuwa akiishi katika eneo moja la gorofa kwa miaka miwili.
"Lakini bado wananiuliza ninafanya nini ndani ya jengo langu," alisema.
"Inaudhi sana."
"Udhalilishaji huu wa mara kwa mara unakatisha tamaa zaidi, kwani nachangia kwa uaminifu mkubwa katika jamii hii kama mtu mwenye kipato kikubwa ambaye analipa kodi nyingi," aliongeza.
Wananchi wa daraja la pili
Sheria ya Ufaransa ya 1978 ilipiga marufuku kukusanya data kuhusu rangi, kabila au dini ya mtu, jambo ambalo hufanya iwe vigumu kuwa na takwimu pana kuhusu ubaguzi.
Lakini kijana "anayetambuliwa kama mtu mweusi au Mwarabu," ana uwezekano wa kuulizwa kitambulisho mara 20 zaidi ya watu wengine, mchunguzi wa haki za Ufaransa alipeleleza mnamo 2017.
Shirika la Ufuatiliaji wa Ukosefu wa Sawa, linasema kuwa ubaguzi wa rangi unazidi kupungua nchini Ufaransa, huku asilimia 60 ya Wafaransa wakitangaza kuwa "sio wabaguzi hata kidogo."
Likaongeza kusema, anayefanyiwa usaili wa kazi mwenye jina la Kifaransa ana nafasi nzuri ya asilimia 50 ya kupata kazi kuliko wenye jina la Afrika Kaskazini.
Mfaransa-Mualgeria mwenye umri wa miaka 30 ana shahada mbili za uzamili kutoka shule za hadhi ya juu, aliiambia AFP kuwa anaondoka mwezi Juni kufanya kazi huko Dubai kwa sababu Ufaransa imekuwa "tatatizo."
Mfanyabiashara wa benki ya uwekezaji, mtoto wa mfanyakazi wa usafi wa Algeria ambaye alikulia ndani ya Paris, alisema alifurahia kazi yake, lakini alianza kuhisi kuwa alifika ukingoni.
Pia alisema amehisi siasa za Ufaransa zikibadilika kwenda kwenye mkondo wa kulia katika miaka ya hivi karibuni.
"Hali ya hewa nchini Ufaransa kwa kweli imezorota," alisema, akitaja baadhi ya wachambuzi wanaowafananisha watu wote wa asili yake na watu wenye msimamo mkali au wakorofi kutoka katika mitaa ya makazi.
"Waislamu ni wazi kuwa ni raia wa daraja la pili," alisema.
Adam, anayefanya kama mshauri, alisema Waislamu wa Ufaransa waliobahatika zaidi kuhama ni "sehemu ndogo inayoonekana ya mwamba wa barafu."
"Tunapoiona Ufaransa leo, imetuvunja moyo," alisema.