Pope | Photo: AP

Papa Francis ameeleza 'wasiwasi wake mkubwa' juu ya ghasia mpya Mashariki ya Kati iliyofuatia uvamizi wa polisi wa Israel kwenye Msikiti wa Al Aqsa huko Jerusalem Mashariki.

Katika ujumbe wake wa Pasaka siku ya Jumapili, papa, kama anavyofanya siku zote, alitoa wito wa amani katika Mashariki ya Kati. Lakini ombi lake mwaka huu lilifanywa kuwa la dharura zaidi kutokana na ghasia za hivi majuzi huko Jerusalem na makabiliano ya moto ya kuvuka mpaka yaliyohusisha Israel, Lebanon na Syria.

''Ninaeleza wasiwasi wangu juu ya mashambulizi ya siku chache zilizopita ambayo yanatishia hali ya kuaminiana na kuheshimiana inayotarajiwa, inayohitajika ili kuanzisha tena mazungumzo kati ya Waisraeli na Wapalestina, ili amani iweze kutawala katika Jiji hilo Takatifu na katika nchi nzima,” alisema.

Mvutano kati ya Waisraeli na Wapalestina umeongezeka kwa kasi tangu polisi wa Israel walipovamia msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem wiki iliyopita, jambo ambalo lilizua ghadhabu katika ulimwengu wa Kiarabu.

Francis, 86, aliongoza Misa kuu ya siku ya Pasaka katika uwanja wa jua wa St.Peter's Square baada ya baridi isiyo ya msimu ilimlazimu kukosa ibada ya nje siku ya Ijumaa - tahadhari kufuatia kulazwa hospitalini kwa ugonjwa wa bronchitis mwishoni mwa Machi.

Zulia la maua 38,000 lililotolewa na Uholanzi lilipamba uwanja huo kwa ajili ya tarehe muhimu na ya furaha katika kalenda ya liturujia ya Kanisa - kuadhimisha siku ambayo Wakristo wanaamini kwamba Yesu alifufuka kutoka kwa wafu.

Vitengo vya heshima vya Walinzi wa Uswizi wa Vatikani na polisi wa Carabinieri wa Italia - wote wakiwa wamevalia mavazi ya sherehe - walisimama kwa umakini.

Baadae Fransisko alikwenda kwenye ubaraza wa ghorofani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ili kuwasilisha ujumbe na baraka zake za kila mwaka za "Urbi et Orbi" (kwa jiji na ulimwengu), akihutubia umati wa Vatikani unaokadiriwa kuwa 100,000.

Vita vya Urusi-Ukraine na tetemeko la ardhi ya Uturuki

Huko, kutoka sehemu ile ile ambapo alijitokeza kwa mara ya kwanza kwa ulimwengu kama papa katika usiku wa kuchaguliwa kwake mwaka 2013, alizungumza juu ya "giza na utusitusi ambamo, mara nyingi sana, ulimwengu wetu unajikuta umegubikwa", na akamuombea Mungu amani.

Papa Francis aliwataka Warusi kutafuta ukweli kuhusu uvamizi wa nchi yao nchini Ukraine. "Wasaidie watu wapendwa wa Ukraine katika safari yao ya kutafuta amani, na uangaze mwanga wa Pasaka kwa watu wa Urusi," alisema.

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari mwaka jana, Francis angalau mara mbili kwa wiki amekuwa akiitaja Ukraine na watu wake kuwa "walijitoa muhanga" na ametumia maneno kama vile uchokozi na ukatili kuelezea vitendo vya Urusi.

Siku ya Jumapili alimwomba Mungu “kuwafariji waliojeruhiwa na wale wote ambao wamepoteza wapendwa wao kwa sababu ya vita, na awajalie wafungwa warudi salama kwa familia zao.

Fungua mioyo ya jumuiya nzima ya kimataifa kujitahidi kukomesha vita hivi na migogoro na umwagaji damu katika dunia yetu."

Kati ya Misa na usomaji wake wa ujumbe, Francis, akionekana kwa umbo zuri, aliendeshwa katika gari la papa kuzunguka barabara kuu inayoelekea Mto Tiber ili watu wengi zaidi waweze kumwona.

Katika ujumbe wake Francis pia alitaja ukosefu wa utulivu nchini Lebanon, alielezea matumaini kwamba "watu wa Rohingya waliouawa shahidi" wa Myanmar "wanaweza kukutana na haki", na kutoa wito wa misaada zaidi kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mwezi Februari ambalo liliua karibu watu 56,000 nchini Uturuki na Syria.

Katika sehemu ya hotuba ambapo alitaja Nicaragua, papa alimwomba Mungu "awakumbuke wote wanaozuiwa kukiri imani yao kwa uhuru na hadharani".

Uhusiano kati ya serikali na Kanisa Katoliki nchini Nicaragua umedorora sana. Serikali, ambayo imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican, ilipiga marufuku maandamano ya nje ya Wiki Takatifu mwaka huu.

TRT Afrika na mashirika ya habari