Ikulu ya Kremlin ilisema kuwa wajumbe kutoka nchi za Afrika wanaotarajia kuwasilisha mpango wao wa kumaliza mzozo nchini Ukraine watazuru Moscow.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi kwamba Moscow itakuwa tayari kusikiliza "mapendekezo yoyote" ambayo yatasaidia kutatua mzozo huo.
Inakuja siku chache baada ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kutangaza kwamba kundi la viongozi sita wa Afrika wanapanga kusafiri kwenda Ukraine na Urusi "haraka iwezekanavyo" kusaidia kupata suluhu la vita.
Mpango huo uliandaliwa na Zambia, Senegal, Jamhuri ya Kongo, Uganda, Misri na Afrika Kusini, Ramaphosa alisema.
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky walikuwa wamekaribisha mpango huo na "kukubali kupokea ujumbe na wakuu wa nchi za Kiafrika, huko Moscow na Kyiv.
Afrika Kusini ni miongoni mwa mataifa kadhaa ya Afrika ambayo yamesalia kutofungamana na Urusi au Ukraine katika vita hivyo.