Zaidi ya Wapalestina 400,000 wamekimbia makazi yao ndani ya Ukanda wa Gaza huku kukiwa na kampeni kubwa ya anga ya Israel, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu ilisema Jumamosi.
"Watu wengi hawana maji safi ya kunywa baada ya mfumo wa kusafisha maji kufungwa na Israel," Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema katika taarifa yake.
"Kama suluhisho la mwisho, watu wanatumia maji yenye chumvichumvi kutoka kwenye visima vya kilimo, na hivyo kusababisha wasiwasi mkubwa kuhusu kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na maji," iliongeza.
Jeshi la Israel liliwaonya wakaazi milioni 1.1 kaskazini mwa Gaza kuhama siku ya Ijumaa "ndani ya saa 24" na kuelekea kusini.
Kampeni ya kutumia nguvu
OCHA ilisema makumi ya maelfu ya wakaazi wanakadiriwa kukimbilia kusini kufuatia agizo hilo.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa haitawezekana kwa Wapalestina huko Gaza kutii amri ya kuondoka kaskazini bila "matokeo mabaya ya kibinadamu."
Vikosi vya Israel vilianzisha kampeni endelevu na ya nguvu dhidi ya Ukanda wa Gaza kujibu mashambulizi ya kijeshi ya kundi la Palestina Hamas katika maeneo ya Israel.
Mzozo huo ulianza Jumamosi iliyopita wakati Hamas ilipoanzisha Operesheni 'Flood Al-Aqsa' - shambulio la kushtukiza la pande nyingi likiwemo safu ya kurusha roketi na kujipenyeza ndani ya Israel kupitia nchi kavu, baharini na angani.
Hamas ilisema operesheni hiyo ni ya kulipiza kisasi kuvamiwa kwa Msikiti wa Al-Aqsa katika Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na kuongezeka kwa ukatili wa walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Jeshi la Israel kisha lilianzisha Operesheni ya 'Iron Sword' dhidi ya malengo ya Hamas ndani ya Ukanda wa Gaza.
Mwitikio huo umeenea hadi katika kukata maji na usambazaji wa umeme hadi Gaza, na kuzidisha hali ya maisha katika eneo ambalo limekuwa chini ya mzingiro tangu 2007.
Zaidi ya watu 3,300 wameuawa tangu kuzuka kwa mzozo huo, wakiwemo Wapalestina 1,900 na Waisrael 1,400.