Shehena zaidi za nafaka zaondoka Ukraine kufuatia makubaliano yaliyoafikiwa Istanbul

Meli nne zaidi zimeondoka Ukraine kama sehemu ya makubaliano yaliyoafikiwa nchini Turkiye kurejelea usafirishaji wa nafaka, Wizara ya Ulinzi ya Turkiye imethibitisha hilo. Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo, meli zingine tisa ziliondoka siku ya Ijumaa baada ya kufunguliwa kwa bandari tatu za bahari nyeusi zilizokuwa zimefungwa kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tangu mwezi Februari.

Aidha majadiliano yanaendelea kurefusha mkataba wa usafirishaji huo baada ya tarehe ya mwisho ambayo ni tarehe 19 Novemba. Inasadikiwa pana uhitaji mkubwa pia wa kusafirisha nafaka ya Urusi pamoja na mbolea. Mkataba uliotiwa saini na mataifa hayo tatu chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa unaruhusu usafirishaji kwa siku 120 tu.

Hakuna pingamizi la kurefusha mkataba

Rais wa Turkiye Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa haoni pingamizi lolote la kurefusha mkataba kwa lengo kuendeleza usafirishaji wa nafaka na mbolea.

“Hakuna pingamizi kwenye kurefusha mkataba. Niling’amua hili kwenye mazungumzo yangu kwa njia ya simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy jana usiku na vilevile mkutano na Rais wa Urusi Vladimir Putin,” Erdogan aliwaambia wanahabari siku ya Alhamisi aliporejea nyumbani kutoka Azerbaijan.

Hatahivyo baadhi ya mamlaka nchini Urusi zinadai kuwa vikwazo vilivyowekewa Urusi na mataifa ya magharibi vinachelewesha usafirishaji wa nafaka na mbolea licha ya kuwepo kwa mkataba hai.

Tangu kuondoka kwa meli ya kwanza nchini Ukraine tarehe mosi Agosti, meli zingine 365 zimeondoka bandarini na zaidi ya tani milioni 8 za mazao ya kilimo.

Reuters