Na Lulu Sanga
Wengi tumezoea kulisikia jina la Tina Tuner katika masikio yetu, na hii ni Zaidi kwa wale watu wa makamo wenyewe tunasema vijana wa miaka ya 70, 80 walioburudika Zaidi na muziki wake uliokonga nyoyo za mashabiki Amerika ulaya hadi Afrika.
Wengine walienda mbali Zaidi na kuwapa watoto wao jina la mwanamuziki huyo mashuhuri ambaye amefariki jana akiwa na umri wa miaka 83 tu.
Wimbo wake wa ‘What love got to do’ ulipata umaarufu mkubwa na kumpanya kuwa mashuhuri Zaidi miaka ya 80. Lakini hata vijana wa sasa bado wanaburudika na wimbo huo ambao bado unafanya vyema ulimwenguni.
TRT Afrika inazungumza na mmoja wa mashabiki wa kubwa wa mwanamuziki huyo aitwaje Julieta Mwema mkazi wa Dar es salaam Tanzania anasema alivutiwa na Tina Turner ulipotoka wimbo wake wa ‘What love got to do’ na wakati huo alikua mjamzito hivyo alipomzaa mtoto wake waliafikiana na mumewe kumpa mtoto jina la mwanamuziki huyo.
“Nilidhani mume wangu angekataa mpango wangu lakini wala hakuwa na shida aliafiki hivyo nikamwita mwanangu Tina na sasa hivi tinawangu keshakua mtu mzima na familia yake ila nikimtazama ni ukumbusho kwa mapenzi na ujana wangu” anamaliza Julieta
Lakini hebu tupate historia fupi ya mwanamuziki huyo
Jina lake halisi ni Anna Mae Bullock japo tunamfahamu Zaidi kama Tina Turner. Pamoja na kufahamika kama mtunzi na mwimbaji wa muziki, pia alifanya vyema kama mwigizaji wa filamu na mwandishi wa vitabu.
Alizaliwa Marekani mwaka 1939 ambapo alikua na dada zake wawili.Kwakuzaliwa ni raia wa Marekani lakini mwaka 2013 alibadili nyaraka zake na kuwa raia wa uswisi
Akiwa binti mdogo alikua akiimba katika kwaya ya kanisani kwenye kanisa la kibabtisti huko Nutbush Marekani
Aliishi na bibi yake ambaye alikua ameshika sana dini na katika moja ya Makala ya maisha yake inayofahamika kama I, Tina alinukuliwa akisema wazazi wake hawakumpenda na hawakumhitaji.
Katika maisha yake ya ujana na kabla ya kuwa Tina Turner alishawahi kufanya kazi za vibarua kama vile nesi msaidizi na mfanyakazi wa kazi za ndani.
Katika harakati za kimuziki, safari yake ilianza baada ya kuvutiwa na mwimbaji Ike Turner ambaye alikua akiimba na band ya ‘Kings of rythim’. Sikumoja alipata fursa ya kushika kipaza sauti mbele ya mwimbaji huyo akapewa fursa ya kuimba Zaidi na siku hiyo alibaki akiimba usiku mzima.
Tangu siku hiyo aliendelea kumfunza namna ya kuimba na kutoa burudani.Hivyo wimbo wake wa kwanza kurekodi ilikua ni 1958 uliitwa ‘Boxtop’ na wakati huo jina lake la la stejini alitumia ‘Little Ann’
Aliandika wimbo wake wa ‘a fool in love’ kwaajili ya msanii Art Lassiter lengo ikiwa yeye mwenyewe aimbe kama msaidizi lakini bahati mbaya au nzuri msanii huyo aliyelengwa hakufika. Ikamlazimu Little Anna kurekodi mwenyewe kwani tayari alikua amelipia muda wa studio.
Hapo ndipo maisha yake yalipobadilika. Wimbo huo ulinunuliwa kwa dola $25,000 kama malipo ya awali tu. Hii ikapelekea Ike Tuner kumbatiza jina la stejini “TINA”. Baadae Ike Turner alimuongezea jina lake na mwisho ‘turner’ kisha akamsajili kisheria ili kulinda haki zake endapo mwanamuziki huyo angetaka kujiondoa chini ya menejimenti yake.
Endapo Bullok angeondoka basi jina la Tina Turner bado lingebaki kua hakimiliki ya Ike na angemuweka msanii mwingine yoyote kwa jina hilo hilo.
Hivyo kuanzia hapo Anna Mae Bullock akatambulika rasmi katika jukwaa la muziki kimataifa kama Tina Turner.
Baadae Tina aliolewa na Ike Turner mumewe ambaye walikua wakifanya muziki pamoja. Na baada ya takriban miongo miwili ya kufanya kazi na mume wake aliyemshutumu kwa unyanyasaji waliachana, ambapo Tina alibaki na magari mawili tu pamoja na jina lake.
Baada ya kuachana, Tina aliibuka kama msanii wa kujitegemea na akawa mmoja wa wasanii wa pop wakubwa wa miaka ya 1980 na albamu yake ya ‘Private Dancer’.
Taarifa za kifo chake na wafuasi wake wanavyo omboleza
Taarifa za kifo cha Tina Turner zimetikisa ulimwengu jumatano usiku. Ambapo vyombo mbalimbali vya habari kimataifa vilitangaza taarifa za mwanamuziki huyo kuaga dunia akiwa nchini Uswisi katika umri wa miaka 83
Imeripotiwa kuwa msanii huyo alikuwa na afya dhoofu katika miaka ya hivi karibuni, kwani aligunduliwa na saratani ya utumbo mnamo 2016 na kupandikizwa figo mwaka 2017.
Taarifa za kifo chake zilitangazwa kupitia mtandao wake wa Instagram ambapo iliandikwa:
“Ni kwa huzuni kubwa kwamba tunatangaza kufariki kwa Tina Turner. Kwa muziki wake na shauku yake isiyo na kikomo ya maisha, alivutia mamilioni ya mashabiki ulimwenguni kote na kuwatia moyo nyota wa kesho. Leo tunasema kwaheri kwa rafiki mpendwa ambaye anatuachia kazi yake kuu zaidi: muziki wake. Huruma zetu zote za dhati ziende kwa familia yake. Tina, tutakukumbuka sana”. (© Peter Lindbergh)
Wafuasi wake kutoka maeneo mbali mbali duniani walimiminika katika mitandao ya kijamii kutuma salamu za rambi rambi huku vituo vya redio na televisheni vikicheza nyimbo zake kwa bidi kubwa kumuenzi.
Mwanamitindo naomi Campbell aliandika katika ukurasa wa Instagram “Pumzika kwa amani & nguvu, gwiji na mfano. Hakutakuwa na mwingine. Nina thamini nyakati zangu na wewe”
Shabiki mwingine aliandika kupitia ukurasa wa twiter “Nyota kama huyo na mwanamke wa ajabu. Ulimwengu umepoteza gwiji. Apumzike kwa amani na apae juu kati ya malaika walio mbinguni. Sala nyingi kwa familia yake katika wakati huu wa huzuni sana! #TinaTurner
"Malkia wangu mpendwa, nakupenda bila kikomo," Beyonce aliandika katika ujumbe kwenye tovuti yake rasmi. "Ninashukuru sana kwa msukumo wako, na njia zote ambazo umefungua.
Watu na mashabiki mbalimbali huko Uswisi wamejumuika nje ya nyumba ya msanii huyo kuweka maua kadi na mishumaa kwa lengo la kumuenzi msanii huyo mashuhuri ulimwenguni.
Na huko London katika ukumbi wa Sanaa wa Aldwych mashabiki wa msanii huyo walikusanyika na kuweka maua kadi na mishumaa.