Polisi Pakistan watibua maandamano ya wafuasi wa Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan.

Polisi Pakistan watibua maandamano ya wafuasi wa Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan.

Serikali imetangaza hali ya hatari katika mikoa 4 nchini Pakistan katika jaribio la kuzima ‘ghasia’
Ghasia kati ya polisi na waandamanaji nchini Pakistan kufuatia kukamatwa kwa Imran Khan/ Photo: DPA / Photo: TRT World

Makabiliano makali yametokea katika mji wa Lahore kati ya polisi na waandamanaji wa aliyekuwa Waziri Mkuu Imran Khan.

Waandamanaji hao walikuwa wanapanga kuelekea mjini Islamabad ambako kiongozi wao anazuiliwa tangu alipotiwa nguvuni Jumanne kuhusiana na kesi ya ufisadi inayomkabili.

Kukakmatwa kwake kumezua wasiwasi wa kutokea ghasia kati ya wafuasi wake na polisi huku baadhi wakidai kuwa kuna ‘njama ya kumuua.’

Pakistan, ghasia kati ya polisi na waandamanaji kufuatia kukamatwa kwa Imran Khan. Picha TRT

Mawasiliano ya simu yalifungwa nchini humo kuanzia Jumanne, huku mitandao ya Youtube, Twitter na Facebook ikikatizwa.

Polisi pia wameweka marufuku ya mikusanyiko yoyote na kutangaza hali ya hatari katika mikoa minne mikubwa.

Khan alikamatwa katika majengo ya mahakama kuu, Jumanne na maafisa kutoka shirika la kukabiliana na ufisadi.

Pakistan, waandamanaji wakilalamikia kukamatwa kwa Imran Khan Picha: TRT

Msemaji wa polisi ameambia shirika la Reuters kuwa, kesi ya Khan itasikizwa katika ‘nyumba salama’ ya polisi, anakozuiliwa badala ya kuletwa mahakamani.

Chama cha waziri mkuu huyo wa zamani, Tehreek-e-Insaf (PTI), kimeitisha ‘Kuzima nchi nzima’, kama njia ya kuendeleza tetesi zao dhidi ya serikali.

Wakati huo huo, chama hicho kimetangaza kukamatwa pia kwa katibu wake mkuu Assad Umar, nje ya mahakama huu, Islamabad.

Waandamanaji Pakistan wakikabiliana na polisi 

Inaaminiwa kuwa kukamatwa kwa Khan kumechochewa na matamshi yake kuishutumu jeshi kuwa na njama ya kumuua, na kuwa mkuu wa jeshi ndiye aliyepanga kuondolewa kwake madarakani, jambo ambalo jeshi limekanusha.

Waziri wa kimkoa Ziaullah Langove amesema kuwa mtu mmoja ameuawa Jumapili, na wengine 12 kujeruhiwa wakiwemo maafisa 6 wa polisi katika makabiliano yaliyozuka katika mji wa Quetta, iliyoko kusini mwa nchi.

Imran Khan, waziri wa zamani wa Pakistan aliyekamatwa na polisi

Khan, 70, aliondolewa madarakani mwezi Aprili 2022, kupitia kura ya Imani bungeni na tangu wakati huo amekuwa akisukuma kufanywa uchaguzi wa mapema.

Zaidi ya kesi 100 zimefunguliwa dhidi ya Khan tangu alipoondolewa uongozini baada ya miaka minne kama waziri mkuu.

Iwapo atakutwa na hatia, huenda Khan azuiwe kabisa kushikilia afisi yoyote ya umma.

Pakistan inapanga kufanya uchaguzi mwezi Novemba.

TRT Afrika