Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul Uturuki
Mzozo mpya umeibuka duniani, kati ya Iran na Israel. Baraza la Umoja wa mataifa la usalama liliitisha mkutano wa dharura siku ya Jumapili kujadili swala hili ambalo wataalamu wanasema lisipotatuliwa litasababisha vita.
Siku ya 13 Aprili 2024, Iran ilianza mfululizo wa mashambulizi Israel. Iran ilifyatua zaidi ya makombora 300 na ndege zisizo na rubani.
Hata hivyo makombora hayo yalidhibitiwa na Israel kwa msaada wa Marekani, Jordan na Uingereza. Kwa mujibu wa jeshi la Israel, watu 12 walijeruhiwa.
Mzozo umetokana na nini?
Iran ilisema shambulio lake ni majibu kwa shambulio la anga la Aprili 1 la Israel kwenye jengo la ubalozi mdogo wa Tehran katika mji mkuu wa Syria, Damascus . Shambulio hilo liliwauwa maafisa saba wa kijeshi wa Iran.
Mashambuliano kama haya ya kijeshi hayajawahi kushuhudiwa na wataalamu wanasema huenda ikazua ongezeko ya uhasama kati ya nchi hizi mbili.
Shambulio kati ya nchi hizi mbili linaonekana kuongeza mgawanyo mkubwa huku nchi kadhaa zikionekana kuikashifu Iran kwa ukali ilhali hazikuweka jitahada hiyo wakati Israel ilivyoshambulia ubalozi wa Iran tarehe moja Aprili.
Siku ya Jumapili, Marekani ilisema kwamba inasimama kidete na Israel lakini haitajiunga na mashambulizi yoyote ya Israel dhidi ya Iran, huku Rais Joe Biden akimuonya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu "kufikiri kwa makini" kuhusu ongezeko lolote la kivita.
Ufaransa na Uingereza pia walitoa wito kwa serikali ya Benjamin Netanyahu kuzuia kuongezeka kwa mgogoro huo.
Urusi imesema mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel yalitokea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kwa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua stahiki pale Israel ilipoishambulia Iran .
Kamati ya vita nchini Israel iliyoundwa baada ya mashambulizi ya Iran inakubaliana kuwa ni lazima kujibu shambulio la Iran, lakini halijaamua ni lini au vipi haya yatafanyika .
Iran nayo imesema imemaliza kulipiza kisasi lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amirabdollahian alionya kuwa iwapo kutatokea shambulio jingine dhidi ya nchi yake, majibu yatakuwa makubwa zaidi.
Huu ni mvutano kati ya nchi mbili zinazotambulika duniani kwa uimara na ubora wa majeshi yao huku Iran ikiwa na silaha za nyuklia. Nchi hizo mbili zilikuwa na uhusiano mzuri hadi mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 nchini Iran.
Iran haitambui uwepo wa Israel. Umoja wa Mataifa unasema lazima ziafikiane kwa ajili ya kupinga vita katika eneo la nchi za mashariki ya kati.
Jitihada za kidiplomasia zimeanza kwa ajili ya kufifisha mvutano kati ya Iran na Israel, kwani tayari kuna vita vingine vinavyoendelea Gaza ambavyo vilianza mnamo Oktoba 7 mwaka 2023.
Mashambulizi ya Israel katika eneo la Gaza yameua takriban watu 33,729 Gaza. Dunia sasa inaangalia kuona kama mvutano kati ya Israel na Iran utaisha?