Mahakama ya Korea Kusini ilitoa kibali kwa mamlaka siku ya Jumanne kumzuilia Rais aliyeondolewa madarakani Yoon Suk Yeol katika uchunguzi wa jinai juu ya agizo lake la sheria ya kijeshi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa rais wa nchi hiyo kukamatwa.
Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi kwa Viongozi wa Vyeo vya Juu (CIO) ilithibitisha Mahakama ya Wilaya ya Seoul Magharibi iliidhinisha hati ya kukamatwa iliyoombwa na wachunguzi juu ya hatua ya Yoon kujitangazia sheria ya kijeshi iliyotibuka.
Yoon, ambaye amesimamishwa kazi, anakabiliwa na uchunguzi kwa madai kwamba alikuwa kiongozi wa uasi, moja ya mashtaka machache ya jinai ambayo rais wa Korea Kusini hana kinga ya ofisi ya Rais.
Kando, kesi yake ya kuondolewa madarakani inasikilizwa katika Mahakama ya Katiba.
Hati ya kukamatwa kwa rais aliye madarakani haijawahi kutokea, na inazidisha mzozo wa kisiasa ambao umeikumba Korea Kusini, nchi ya nne kwa uchumi mkubwa barani Asia
Waziri Mkuu Han Duck-soo, ambaye alichukua nafasi ya Yoon kama kaimu rais, pia ameondolewa na bunge, ambalo linaongozwa na upinzani.
Waziri wa Fedha Choi Sang-mok, ambaye alichukua wadhifa wa kaimu rais baada ya kuondolewa madarakani kwa Han, amekuwa akikabiliana na ajali ya Jumapili ya ndege ya Jeju Air 7C2216, ambayo iliua watu 179 katika maafa mabaya zaidi ya anga katika ardhi ya Korea Kusini.
Hati ya sasa ya kukamatwa inaweza kutumika hadi Januari 6, na inawapa wapelelezi saa 48 pekee kumshikilia Yoon baada ya kukamatwa. Wachunguzi basi lazima waamue ikiwa wataomba kuongezewa muda wa kumzuilia au kumwachilia.
Mara baada ya kukamatwa, Yoon anatarajiwa kuzuiliwa katika Kituo cha Kizuizi cha Seoul, shirika la habari la Yonhap lilisema, likitaja maelezo ya CIO.
Yoon Kab-keun, wakili wa rais aliyetimuliwa, alisema hati ya kukamatwa ilikuwa kinyume cha sheria na ni batili kwa sababu CIO haikuwa na mamlaka chini ya sheria ya Korea Kusini kuomba kibali.
Wafuasi wa Yoon waandamana
Alisema timu ya wanasheria wa rais itawasilisha zuio katika Mahakama ya Katiba kusitisha hati hiyo.
Mamia ya wafuasi wa Yoon walikusanyika nje ya makazi yake Jumanne kupinga kibali hicho, baadhi wakizozana na polisi.
Mahakama ya wilaya ilitoa kibali hicho kutokana na uwezekano kwamba Yoon hatajibu wito bila sababu zinazokubalika, na kukiwa na sababu kubwa ya kumshuku Yoon kwa uhalifu, Yonhap alisema. Mahakama ilikataa kutoa maoni.
Utaratibu wa kufuatwa
Haikuwa wazi ni lini au vipi hati ya kukamatwa kwa Yoon itatekelezwa. Idara ya usalama ya rais wa Korea Kusini ilisema katika taarifa siku ya Jumanne kwamba itashughulikia agizo la kukamatwa kwa mujibu wa taratibu zinazofaa.
Mahakama pia iliidhinisha kibali cha upekuzi kwa makazi ya Yoon, CIO ilisema.
Hapo awali, polisi walijaribu lakini walishindwa kuvamia ofisi ya rais kama sehemu ya uchunguzi, kutokana na kikosi cha usalama ya rais kuwazuia kuingia.
Kufikia sasa, waendesha mashtaka wamewafungulia mashtaka maafisa watatu wakuu wa ulinzi kuhusiana na sheria ya kijeshi ya Yoon.
Waziri wa zamani wa Ulinzi Kim Yong-hyun, ambaye kesi yake itaanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza Januari 16, pamoja na Yeo In-hyung, mkuu wa Kamandi ya Kukabiliana na Ujasusi ya Ulinzi na Lee Jin-woo, kamanda wa Kamandi ya Ulinzi Mkuu, wamefunguliwa mashtaka, huku wengine wengi wakitarajiwa kufuata.
Wachunguzi walivamia ofisi za jeshi la kukabiliana na kijasusi siku ya Jumanne kama sehemu ya uchunguzi wao.
Choi alitoa wito wa kuwepo kwa maelewano na umoja wa kitaifa na imani kwa serikali katika hotuba ya Mwaka Mpya siku ya Jumanne, akisema nchi "iko katika hali mbaya sana."