Takriban watu 167 wamethibitishwa kufariki na watu wawili tu - wote ni wafanyakazi wa ndege - waliokolewa, shirika la zima moto la Korea Kusini limesema, baada ya ndege ya Jeju Air kuanguka ikiwa na watu 181.
"Hadi sasa wawili waliokolewa, 167 wamethibitishwa kufariki," Shirika la Kitaifa la Zimamoto lilisema katika taarifa Jumapili, huku shughuli ya kuwatafuta na kuwaokoa ikiendelea.
Ndege ya Jeju Air iliyokuwa na abiria 181, wakiwemo wafanyakazi sita, ilishika moto wakati ikitua baada ya kuripotiwa kukabiliwa na matatizo ya vifaa vya kutua karibu saa 9.07 kwa saa za huko katika kaunti ya Muan - kilomita 288 (maili 179) kusini magharibi mwa mji mkuu wa Korea Kusini wa Seoul, kulingana na Yonhap News.
Ndege hiyo yenye injini mbili, iliyokuwa ikirejea kutoka Bangkok, iliacha njia na kugongana na uzio kabla ya kugonga ukuta katika mlipuko wa moto.
Picha za vyombo vya habari vya ndani zilionyesha ndege hiyo ikiteleza kwenye njia ya kurukia ndege, ikiwa imeteketea kwa moto na vifusi.
Abiria na mhudumu walipatikana wakiwa hai katika sehemu ya mkia wa eneo hilo huku juhudi za uokoaji zikiendelea ingawa mamlaka ilisema kwamba idadi ya waliojeruhiwa huenda itaendelea kuongezeka.
Wengi wa abiria walikuwa Wakorea pamoja na raia wawili wa Thailand.
Afisa mmoja wa uwanja wa ndege alisema mamlaka inalenga katika kuwaokoa wale waliokwama kwenye mabaki hayo.
Kumezwa na moto
Kaimu Rais Choi Sang-mok alitoa wito wa kukusanywa kwa rasilimali zote ili kuokoa abiria.
"Mashirika yote yanayohusiana... lazima yakusanye rasilimali zote zilizopo ili kuokoa wafanyikazi," aliagiza maafisa katika taarifa.
Choi aliitisha kikao cha dharura na wajumbe wa baraza la mawaziri kujadili shughuli za uokoaji na majibu, ofisi yake ilisema, na kuongeza kuwa yuko njiani kuelekea Muan.
Ni ajali ya kwanza mbaya katika historia ya Jeju Air, mojawapo ya ndege kubwa zaidi za gharama nafuu za Korea Kusini, ambayo ilianzishwa mwaka 2005.
Mnamo Agosti 12, 2007, Bombardier Q400 inayoendeshwa na Jeju Air iliyokuwa na abiria 74 ilitoka kwenye njia ya ndege kutokana na upepo mkali katika uwanja wa ndege wa Busan-Gimhae wa kusini, na kusababisha majeraha kadhaa.
Sekta ya usafiri wa anga ya Korea Kusini ina rekodi thabiti ya usalama, wataalam wanasema.
Mwaka jana, abiria alifungua njia ya kutokea kwa dharura kwenye ndege ya shirika la ndege la Asiana Airlines ilipokuwa ikijiandaa kutua, huku ndege hiyo ikitua salama lakini watu kadhaa walilazwa hospitalini.