Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ndege la Korea Kusini Jeju Air amewaomba radhi waathiriwa wa ajali ya ndege iliyosababisha vifo vya takriban watu 167 Jumapili iliyopita.
Katika kikao kifupi na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu Kim E-bae alisema kuwa kuunga mkono wafiwa ni jambo la kipaumbele kwa sasa.
Wakati huo huo, Boeing ilitoa salamu za rambirambi na kusema inawasiliana na Jeju Air ya Korea Kusini baada ya ajali hiyo mbaya.
Ajali hiyo ilihusisha ndege aina ya Boeing 737-800, kulingana na Jeju Air.
Ndege ya Jeju Air iliyokuwa na watu 181 kutoka Bangkok kuelekea Korea Kusini ilianguka siku ya Jumapili ilipowasili, na kugongana na kizuizi na kuwaka moto, huku watu wawili pekee walionusurika wakiokolewa hadi sasa.
Mgongano na ndege wanaopaa na hali mbaya ya hewa ilitajwa na mamlaka kama sababu zinazowezekana za ajali hiyo iliyowatupa abiria nje ya ndege na kuiacha "karibu kuharibiwa kabisa", kulingana na maafisa wa zima moto.
Video ilionyesha ndege ya Jeju Air ikitua kwa tumbo bila magurudumu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan, ikiserereka kutoka kwenye njia ya ndege huku moshi ukitoka kwenye injini, kabla ya kuangukia ukuta na kulipuka kwa moto.