Makumi kwa maelfu ya Waisraeli wameandamana dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu huku vita vya Israel dhidi ya Gaza vikifikia hatua ya nusu mwaka.
Waandalizi wa maandamano ya Jumamosi walisema takriban watu 100,000 walikusanyika katika njia panda ya Tel Aviv iliyopewa jina la "Demokrasia Square" tangu maandamano makubwa ya kupinga mageuzi yenye utata ya mahakama mwaka jana.
Wakiimba "uchaguzi sasa", waandamanaji walimtaka ajiuzulu wakati vita huko Gaza vikiingia mwezi wake wa saba Jumapili, waandishi wa AFP waliripoti.
Mikutano ya hadhara pia ilifanyika katika miji mingine, huku kiongozi wa upinzani wa Israel Yair Lapid akishiriki katika moja huko Kfar Saba kabla ya kuondoka kwake kwa mazungumzo huko Washington.
"Hawajajifunza chochote, hawajabadilika," alisema katika mkutano huo.
"Mpaka tuwatume nyumbani, hawataipa nchi hii nafasi ya kusonga mbele."
Mapigano kati ya polisi na waandamanaji
Vyombo vya habari vya Israel vimesema mapigano yalizuka kati ya waandamanaji na polisi katika mkutano wa Tel Aviv na polisi walisema kuwa muandamanaji mmoja amekamatwa.
Baadaye, waandamanaji huko Tel Aviv waliunganishwa na familia za mateka wa Gaza na wafuasi wao.
Hapo awali, jeshi lilitangaza kuwa wanajeshi waliupata mwili wa mateka waliotekwa nyara na Hamas mnamo Oktoba 7.
Kupatikana kwa mwili wa Elad Katzir kunafikisha idadi ya miili 12 ya mateka ambayo jeshi linasema kuwa limeleta nyumbani kutoka Gaza wakati wa vita.
Shambulio la Hamas lilisababisha vifo vya watu 1,170 kusini mwa Israel, wengi wao wakiwa raia, kwa mujibu wa takwimu za Israel.
Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel huko Gaza yamesababisha vifo vya Wapalestina 33,137 wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kwa mujibu wa wizara ya afya katika eneo linaloongozwa na Hamas.
Takriban Waisraeli 250 na wageni walichukuliwa mateka na Hamas mnamo Oktoba 7.
Jeshi linasema 129 bado wanazuiliwa huko Gaza, wakiwemo 34 wanaokisiwa kufariki.
Waandamanaji wataingia barabarani tena siku ya Jumapili, huku maandamano yakipangwa mjini Jerusalem.