Uchaguzi Somalia umekubaliwa ufanyike mara moja kila baada ya miaka mitano Picha: Ikulu  Somalia

Kwa mara ya kwanza, Viongozi wa Somalia wakiwemo Rais wa zamani, Mawaziri wakuu wa zamani, Maspika wa zamani na wanasiasa wengine wamekutana mjini Mogadishu kwa mashauriano juu ya mfumo mpya wa uchaguzi na kuamua mustakabali wa taifa hilo.

Mkutano huo ulioitishwa na kuongozwa na Rais Hassan Sheikh Mohamud, umeanza leo mjini Mogadishu, ili kujadili mchakato wa uchaguzi wa mfumo wa uongozi wa Rais na Makamu wa Rais watakaochaguliwa kwa pamoja na raia wa Somalia kupitia kura ya moja kwa moja kuzingatia mfumo wa vyama vingi.

Miongoni mwa viongozi wanaoshiriki ni Rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed, Mawaziri Wakuu wa zamani Mohamed Hussein Roble, Hassan Ali Khaire, Abdiweli Mohamed Ali Gas, Omar Abdirashid Sharmarke, Ali Mohamed Gedi na Maspika wa Zamani wakiwemo Mohamed Mursal Shekh, na Mahmoud Osman Jawari. Naibu Waziri Mkuu wa zamani Ridwan Hirsi Mohamed pia anashiriki mkutano huo.

Mfumo mpya wa Uchaguzi unaopendekezwa Somalia ni upi?

Kulingana na mojawapo ya ibara ya makubaliano hayo, wajumbe wa bunge la wananchi watachaguliwa moja kwa moja kwa wapigiwa kura kupitia njia ya siri unaozingatia mfumo wa vyama vingi vya siasa.

  • Uchaguzi utafanyika mara moja kila baada ya miaka mitano.

  • Uchaguzi wa Rais na Makamu wake utafanyika Novemba 2024.

  • Uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika 30 Juni, 2024.

Ingawa hajashiriki mkutano huo, Rais wa zamani wa Somalia Mohamed Abdullahi 'Farmaajo' alikaribisha makubaliano yaliyoafikiwa na viongozi wa Baraza la Taifa la Ushauri mapema mwezi Mei.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ameahidi kuwa lengo la mashauriano ni kuiwezesha Somalia kuwa na mfumo wa Uchaguzi huru, salama, wenye haki na uadilifu.

Mkutano huu utaendelea hadi Julai 15 huku viongozi hao wakitarajiwa kutoa mtazamo wao kuhusu makubaliano ya viongozi wa Somalia maarufu "mkutano wa Baraza la viongozi wa kitaifa la Ushauri uliofanyika mnamo mwezi Mei mwaka huu.

TRT Afrika