Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ndiye mwenyeji wa mkutano huo / Picha: Reuters

Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amefungua rasmi mkutano wa kimataifa wa usalama wa chakula ulionza rasmi mjini London leo Jumatatu.

Mkutano huo umewaleta pamoja wawakilishi kutoka zaidi ya mataifa 20, miongoni mwao, Somalia, UAE, Brazil, Pakistan, Yemen, Ethiopia, Tanzania, Malawi, na Msumbiji ili kujadili uimarishaji wa jitihada za kushughulikia usalama wa chakula.

Uingereza inatarajiwa kuzindua mpango wake wa muda mrefu wa maendeleo ya kimataifa.

Mkutano huo, ni mpango wa ushirikiano kati ya Uingereza, Somalia, UAE, msingi wa mfuko wa uwekezaji wa watoto na wakfu wa Bill na Melinda Gates, unatarajiwa kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 20.

Aidha, Uingereza imetangaza kutoa hadi pauni milioni 100 ( dola milioni 125) katika ufadhili wa kibinadamu kwa nchi zilizoathiriwa zaidi na ukosefu wa chakula zikiwemo Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini na Afghanistan, na kwa nchi zilizoathiriwa na majanga ya kibinadamu kama vile vimbunga vinavyohusiana na hali ya hewa na ukame kama Malawi.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud ni mmoja wa viongozi kutoka mataifa yaliyoathirka zaidi na usalama wa chakula kufika nchini humo.

Rais huyo wa Somalia, anatarajiwa kuhutubia mkutanoi huo, utakaohutubiwa pia na Waziri wa Milki za Kiarabu UAE wa mabadiliko ya tabia nchi na Mazingira Mariam Almheiri na Sir Chris Hohn wa Shirika la kimataifa la CIFF.

Uingereza imesema kuwa itapiga jeki juhudi za kukabiliana na utapiamlo wa watoto kwa kutoa mchango sawa wa fedha na rasilimali zitakazotengwa na serikali za nchi zilizoathirika zaidi kama vile Uganda, Ethiopia na Senegal kukabiliana na suala hilo, hayo ni kwa mujibu wa Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO).

TRT Afrika na mashirika ya habari