Wanawake na watoto walikuwa miongoni mwa walioathiriwa katika shambulio la hospitali. / Picha: AA

Serikali ya Somalia kupitia wizara yake ya mambo ya nje, imetoa taarifa ya kulaani vikali shambulio la bomu dhidi ya hospitali ya Al- Ahli Baptist eneo la Gaza.

Taarifa hiyo ya mapema siku ya Jumatano ilisema, "Jamhuri ya shirikisho la Somalia inalaani kwa maneno makali shambulio la bomu la hospitali ya Ahli Baptist huko Gaza, lililosababisha majeruhi na vifo vya zaidi ya raia 500 wa Palestina, wakiwemo watoto na wanawake.

Wakati huo huo, Somalia imesisitiza kwamba inailaumu Jeshi la Israel kwa kutekeleza shambulio hilo huku ikiitaka Israel kufungua mipaka kwa ajili ya Wapalestina mara moja.

"Jeshi la Israeli ndilo linalobeba jukumu. Mamlaka ya israel inapaswa kufungua njia salama na mipaka kwa ajili ya misaada ya kibinadamu ili kufikia Ukanda wa Gaza uliozingirwa,'' ilisema taarifa hiyo.

Aidha, serikali ya Somalia imetoa wito wa uingiliaji wa kimataifa ili kukomesha ukiukaji wazi wa haki za kibinadamu na mauaji ya ya kiholela ya Wapalestina huko Gaza.

"Kile ambacho Israeli inafanya huko Gaza kinachukuliwa kuwa ukiukaji wa wazi na usio na msingi na kitendo ambacho kinakinzana na sheria na kanuni za kimataifa na maadili ya kibinadamu, pamoja na sheria za kimataifa, " taarifa ilisema.

TRT Afrika