Daktari akiwa ameshikilia bendera wakati wa maandamano ya kudai haki kufuatia ubakaji na mauaji ya mhudumu wa afya katika hospitali ya Kolkata, New Delhi, India, Agosti 19, 2024. / Picha: Reuters

Na Nilosree Biswas

Katika siku chache zilizopita, mvua imenyesha bila kukoma huko Kolkata, mji mkuu wa jimbo la West Bengal nchini India.

Lakini hilo halijazuia chama cha West Bengal Junior Doctors Front na raia wa tabaka mbalimbali kushiriki katika maandamano makubwa ya kudai haki kwa daktari ambaye alibakwa na kuuawa katika Chuo cha Matibabu cha RG Kar mwezi uliopita.

Ni zaidi ya siku 36 zimepita tangu daktari huyo kuuawa katika chuo kimoja kikongwe zaidi cha matibabu nchini.

Tangu wakati huo, maandamano yameshika kasi Kolkata, huku waandamanaji wakidai haki na kufanikiwa kusababisha kutimuliwa kwa kamishna wa polisi wa jiji hilo na maafisa wa afya wa serikali ya jimbo.

Hasira ya umma imeenea kote nchini, na pia kwa miji 25 kupitia Uropa na Amerika Kaskazini.

Katika hotuba ya Siku ya Uhuru mwezi uliopita, Waziri Mkuu Narendra Modi aligusia uhalifu huo, akisema serikali za majimbo zinapaswa kuingiza hofu ya adhabu kwa wahalifu na kuongeza imani kwa jamii. Walakini, chama chake cha BJP kinaonekana kukabiliana na shida yake ya ubakaji.

Bado, kile kilichotokea usiku wa Agosti 9 hakijafungua tu lango la ghadhabu, lakini pia ilifungua tena makovu ya siku za nyuma, na kuwalazimisha Wahindi kuuliza tena maswali magumu kuhusu utamaduni wa ubakaji, ugonjwa ambao umeshika jamii yetu kwa muda mrefu sana.

Katika mwezi uliopita, matukio muhimu yamefanyika nchini India.

Ya kwanza, Mahakama Kuu ya India imeanza kusikiliza kesi ya Kolkata, na Ofisi Kuu ya Upelelezi (CBI) imechukua mamlaka juu ya suala hilo.

Wakati huo huo, mahakama ya wilaya ya Siliguri (katika Bengal Kaskazini) imetangaza hukumu ya hatia katika kesi ya ubakaji na mauaji iliyotokea katika eneo la Matigara tarafa ya Siliguri, takriban mwaka mmoja uliopita. Mhusika alihukumiwa kifo.

Zaidi ya hayo, kesi zaidi za ubakaji zinaendelea kuripotiwa kote nchini, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa mwanamke mchana huko Ujjain, Madhya Pradesh, na ubakaji na mauaji ya msichana wa miaka 14 wa Dalit huko Bihar, pamoja na ripoti ya kwamba wanafunzi wawili wa shule ya chekechea (wasichana) walikuwa wamenyanyaswa kingono na wafanyikazi wa shule (waliohusika na usafishaji) huko Badlapur, Maharastra.

Na haya ni matukio tu ambayo yamegonga vichwa vya habari.

Kutokana na matukio haya yote yanayofuatana, ni sawa kuhitimisha kwamba India iko katika hali ngumu na ya kufadhaisha, kuna mambo mawili yana ukweli.

Kwanza, kwamba taratibu za kutii sheria zipo, mahakama inafanya kazi kuelekea kutoa haki, na hukumu na adhabu hutamkwa na kutekelezwa.

Pili, ukatili wa kijinsia na ubakaji bado unaendelea. Kwa hivyo tatizo ni nini, na kwa nini India haiwezi kulitatua? Yaliyotokea hivi karibu huenda ikawa na majibu.

Jaribio la kuleta mageuzi

Mnamo Desemba 16, 2012, mwanafunzi wa tibamaungo mwenye umri wa miaka 23 alibakwa na wanaume sita katika basi lililokuwa likienda huko New Delhi.

Mwathiriwa, aliyepewa jina la utani Nirbhaya, au asiyeogopa, katika ripoti za vyombo vya habari, kwa sababu sheria ya India inakataza kumtaja mwathiriwa wa ubakaji kwa jina lake la kweli, alikufa kwa majeraha siku chache baada ya shambulio hilo.

Uhalifu huo ulikuwa ni unyanyasaji wa kijinsia ambao ulileta mawimbi ya mshtuko kote nchini, na kusababisha hasira kubwa kwa miezi kadhaa, na kuvutia hisia za kimataifa na kusababisha mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa sheria mpya ya kupinga ubakaji ambayo inaweka vikwazo vya adhabu ya kifo kwa uhalifu huo.

Wanaume wanne waliohukumiwa walipatikana na hatia na kunyongwa mnamo Machi 20, 2020 katika jela ya Tihar.

Wa tano alijiua wakati akitumikia kifungo chake na huku mhalifu mwenye umiri mdogo ambaye alikuwa chini ya umri wa miaka 18 wakati wa uhalifu aliachiliwa baada ya kifungo cha miaka mitatu, akihudumia kiwango cha juu chini ya sheria ya watoto nchini India.

Mnamo mwaka wa 2018, kesi nyingine mbaya ilifunuliwa: ubakaji na mauaji ya mtoto mdogo (mtoto wa kike) huko Indore, Madhya Pradesh. Hii ilisababisha kesi hio kufuatiliwa kwa haraka kaitika muda wa wiki tatu, kesi ya haraka zaidi kuwahi kutokea katika kesi ya ubakaji nchini India baada ya uhuru, huku mhalifu huyo wa kiume mwenye umri wa miaka 26 akipatikana na hatia na kuhukumiwa kifo.

Ujumbe uliotumwa kupitia kesi zote mbili ulikuwa mkali na wazi, lakini matukio ya udhalilishaji, ubakaji na mauaji yanaendelea kukithiri kwa miaka mingi.

Pia ukiangalia kabla ya robo ya tatu mwaka huu. Hukumu nyingi za kesi mbalimbali zimetangazwa na hukumu kutolewa, ikiwa ni pamoja na hukumu ya kifo, na zote zina uwezekano wa kutekelezwa.

Katika nchi ambapo mchakato wa kisheria unachukua miaka mingi, maamuzi yanapongezwa na kutoa mwanga wa matumaini.

Walakini, ukweli huko mashinani unabaki kuwa mbaya. Data ya kimataifa na ya kitaifa inaonyesha picha za kutisha za matukio ya ukatili dhidi ya wanawake, ikiwa ni pamoja na ubakaji na mauaji. Tazama miaka mitatu iliyopita pekee.

Kulingana na Ripoti ya Ofisi ya Kitaifa ya Uhalifu (NCRB), ambayo ilitoa takwimu 2022 za uhalifu mwishoni mwa 2023, India ilishuhudia kuongezeka kwa asilimia 4 ya uhalifu dhidi ya wanawake ikiwa ni pamoja na ubakaji, mauaji, vifo vya mahari, unyanyasaji na mashambulizi ya tindikali.

Mnamo 2020, kulikuwa na kesi 371,503 zilizosajiliwa za uhalifu dhidi ya wanawake.

Tangu wakati huo, kumekuwa na ongezeko la kutisha la viwango vya uhalifu huku kesi 445,256 zikiorodheshwa mnamo 2022.

Kesi za ubakaji zilizosajiliwa mwaka wa 2021 zilifikia 31,677, au wastani wa kesi 87 kwa siku - ongezeko la asilimia 19.34 kutoka 2020.

Hasa, hukumu zinazohusiana na ubakaji zilizosajiliwa kati ya 2018-2022 ni asilimia 28 pekee.

Mwaka jana, Taasisi ya 'Georgetown Women, Peace and Security Index', iliorodhesha India vibaya, na kuiweka katika nafasi ya 128 kati ya nchi 177 katika masuala ya usalama, haki na ushirikishwaji wa wanawake.

Mzunguko mbaya

Kwa hivyo India inapaswa kufanya nini kuhusu tatizo lake la ubakaji?

Mapema mwaka huu, Jimbo la Bengal Magharibi lilipitisha Mswada wa 'Aparajita'. Mswada huo unaangazia sheria ua vifungu vipya zaidi vinavyohusiana na makosa ya ngono, ikiwa ni pamoja na ubakaji. Mswada huo unanuiwa kuimarisha zaidi ulinzi wa watoto na wanawake huko Bengal Magharibi. Majimbo mengine yanafanya kazi kupitisha sheria kwa njia sawa na kadhalika mahakama kote nchini inaongeza juhudi za kupata haki.

Lakini kwa nini ubakaji bado unasalia kuwa uhalifu wa kawaida dhidi ya wanawake nchini India? Kwa nini India inajitahidi kukomesha utamaduni wake wa ubakaji? Jibu lake si rahisi.

Katika nchi iliyogawanyika sana, ubakaji unamaanisha zaidi ya uhalifu wa kijinsia. Ni kitendo kinachotumiwa kulipiza kisasi ndani ya siasa za tabaka na mizozo ya kibinafsi.

Hilo linaturudisha kwenye mfumo wa kuonyeshana ubabe wa India na chuki iliyokita mizizi, ambapo kuwanyanyasa na kuwatesa wanawake inaruhusiwa na ambapo wanawake huona aibu kwa kubakwa.

Madaktari wadogo waandamana kumtaka kamishna wa polisi wa jiji kujiuzulu na kulaani ubakaji na mauaji ya daktari, huko Kolkata mnamo Septemba 2, 2024. /Picha: AFP.

Kwa kuzingatia dosari hii ya kijamii, hakuna uwezekano kwamba idadi ya ubakaji itapungua au kukoma kabisa. Hii ndiyo sababu pia hukumu za kihistoria kama ilivyo kwa Nirbhaya zimeshindwa kuanzisha mabadiliko yoyote yanayoonekana. Inaonyesha kutokuwepo kwa woga wa sheria, kwani hukumu ya maisha wala adhabu ya kifo haiwatishi wahalifu.

Zaidi ya hayo, kuna ucheleweshaji wa taarifa za polisi na usajili wa malalamiko, na hivyo kuzuia utekelezaji wa haraka wa sheria zilizopo dhidi ya makosa ya ngono.

Ni safari ndefu hadi pale utamaduni wa kukabiliana uhalifu huo na ambao hatimaye unaweza kushinda mfumo dume, nguvu za kiume zenye sumu na chuki dhidi ya wanawake nchini India.

Huku kilele cha maandamano ya Kolkata, ni wakati mwafaka wa kuchukua mafunzo kutoka zamani ili kusuluhisha tatizo lililokithiri la uhalifu wa kijinsia katika kila ngazi ya kijamii, kukuza na kuhimiza mazingira yanayozingatia jinsia na usalama wa mazingira.

Vinginevyo, kufanya mabadiliko makubwa chini ya mfumo wa haki ya jinai au kwa sheria kunaweza kufanya kazi kwa muda tu.

Mwandishi, Nilosree Biswas ni mwandishi na mtengenezaji wa filamu ambaye anaandika kuhusu historia, utamaduni, chakula na sinema ya Asia ya Kusini, Asia na diaspora yake.

Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.

Pata habari zaidi kupitia whatsapp channels

TRT Afrika