India imesimamisha huduma zote za utoaji viza kwa raia wa Canada na kuitaka nchi hiyo kupunguza wafanyakazi wake wa kidiplomasia siku ya Alhamisi.
Marufuku hiyo inamaanisha kuwa raia wa Canada ambao bado hawana viza, hawataweza kuingia India hadi pale huduma zitakapoanza tena. Mnamo 202, watalii wapatao elfu 80 wa Canada walizuru India, na kuwafanya kuwa kundi la nne kwa ukubwa, kulingana na Ofisi ya Uhamiaji ya India.
Hii ni baada ya mgogoro kati ya nchi hizo kupanuka baada ya Waziri Mkuu wa Canada kuilaumu India kwa kuwa na uwezekano wa kuhusika katika mauaji ya raia wa Canada.
Wiki hii, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alisema kuwa kulikuwa na "madai ya kuaminika" ya kuhusika kwa India katika mauaji ya kiongozi wa kujitenga wa Sikh ndani ya ardhi ya Canada.
Hardeep Singh Nijjar, raia wa Canada mwenye umri wa miaka 45 ambaye alikuwa akitafutwa na India kwa miaka mingi, aliuawa kwa kupigwa risasi mwezi Juni nje ya hekalu aliloongoza eneo la Surrey, nje ya Vancouver.
Wakati wa mauaji yake, Nijjar alikuwa akiandaa kura ya maoni isiyo rasmi ya Sikh juu ya kujitenga kutoka India.
Hata hivyo, Canada bado haijatoa ushahidi wowote wa kuhusika kwa India katika mauaji hayo.
Madai hayo mazito kutoka kwa Trudeau siku ya Jumatatu yalizalisha uhasama wa kidiplomasia na kupelekea kila nchi kumfukuza mwanadiplomasia. India ilikataa madai hayo na kuyaita ya kipuuzi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India Arindam Bagchi alithibitisha kusimamishwa kwa muda kwa huduma zote za viza kwa raia wa Canada, ikiwemo viza za kielektroniki na viza vilivyotolewa katika nchi zingine.
"Vitisho vya usalama vinavyokabili mabalozi yetu nchini Canada vimevuruga utendaji wao wa kawaida. Aidha, hawawezi kufanikisha maombi ya viza kwa muda. Tutazidi kukagua hali hiyo mara kwa mara," Bagchi aliwaambia waandishi wa habari.
Kwa miaka mingi sasa, India imeikosoa Canada kwa kuwapa uhuru waasi wa Sikh, pamoja na Nijjar. New Delhi ilimshtumu kwa kuwa na uhusiano na ugaidi, jambo ambalo Nijjar alikataa.
Serikali ya India imekuwa ikionya mara kwa mara kwamba waasi wa Sikh wanajaribu kurudi na kushinikiza nchi kama Canada, ambapo Sikhs hujumuisha zaidi ya 2% ya idadi ya watu, kufanya juhudi zaidi za kuwazuia.
Dalili za mpasuko mpana wa kidiplomasia kati ya Canada na India ziliibuka katika mkutano wa Kilele wa Kundi la mataifa 20 yanayoongoza kwa uchumi wa Dunia ulioandaliwa na India mapema mwezi huu.
Uhusiano kati ya Trudeau na Modi kwenye mkutano huo ulionekana kuwa 'mbaya', na siku chache baadaye Canada ilifuta ujumbe wa biashara ulioratibiwa kwenda India. Makubaliano ya kibiashara kati ya wawili hao sasa yamesitishwa.