Canada iliashiria ukurasa mpya katika historia ya nchi hiyo Jumanne kwa kumchagua Spika wa kwanza Mweusi wa Bunge la Uakilishi.
Mbunge wa Liberal Greg Fergus atachukua nafasi ya Anthony Rota ambaye alijiuzulu wiki iliyopita baada ya kumwalika mkongwe wa zamani wa Vita vya Pili vya Dunia ambaye alipigana pamoja na Wanazi (waliomuunga mkono Hitler) kuhudhuria Bunge wakati wa hotuba ya Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine bungeni.
Rota alisema hakufahamu uhusiano wa Wanazi wa Varoslav Hunka, lakini maisha yake ya nyuma yalipojulikana, kosa hilo lilishika vichwa vya habari vya kimataifa na ilikuwa aibu kubwa kwa Canada.
Fergus alikuwa mmoja wa wabunge saba wanaotaka kujaza nafasi ya spika ambayo kimsingi ni kudhibiti mienendo ya wabunge na kuongoza ajenda na kusuluhisha mijadala.
'Rejesha utaratibu na heshima'
Wabunge mara kwa mara hugeuza baraza hilo, maarufu kama 'House of Commons' kuwa jukwaa la kurushiana matusi, kuzozana na kudhalilishana.
Fergus alisema anatumai kurejesha utulivu na heshima kwa chumba.
"Heshima na adabu - nitafanya kazi kwa bidii katika hili na ninahitaji usaidizi wenu nyote kufanikisha hili," Fergus alisema kutoka kwa kiti cha spika katika hotuba kwa wabunge baada ya kuchaguliwa kwa kura ya siri.
"Heshima ni sehemu ya msingi ya kile tunachofanya hapa," alisema. "Tunahitaji kuhakikisha kwamba tunaheshimiana na tunawaonyesha raia wetu mfano huo. Hatuwezi kuwa na mazungumzo isipokuwa kuwe na maelewano ya kuheshimiana."
Waziri Mkuu Justin Trudeau alisema anatumai Fergus amefanikiwa katika azma yake.
"Tulikuchagua ili utusaidie kuwa wastaarabu katika mijadala yetu, ili kutukumbusha sisi sote tuko hapa kwa sababu moja, ambayo ni kuwatumikia Wakanada," Trudeau alisema.
Wakati spika ni mwanachama wa chama cha kisiasa - Fergus, kwa mfano, ni mbunge katika Chama cha Kiliberali cha Trudeau - jukumu hilo si la upendeleo.