Roketi zilizorushwa kutoka kusini mwa Lebanon zimenaswa na Israeli, tarehe 4 Agosti 2024, huku kukiwa na mapigano yanayoendelea ya mpakani kati ya wanajeshi wa Israeli na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon. /Picha: AFP

Na

Hannan Hussein

Wakati ulimwengu ukingoja kuona jinsi Iran itakavyojibu mauaji mawili ya hivi majuzi ya viongozi wakuu yaliyofanywa na Israeli, Marekani inapaswa kupima kwa makini wajibu wake katika kile kitakachotokea baadaye.

Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umekuwa ukijiandaa kwa "mashambulio makubwa" kutoka Iran na washirika wake kufuatia mauaji ya Ismail Haniyeh, kiongozi wa ofisi ya kisiasa wa zamani wa chama cha Hamas aliyeuawa mjini Tehran mwezi uliopita, pamoja na kifo cha kamanda mkuu wa jeshi la Hezbollah, Fuad Shukr huko Beirut.

Ongezeko la msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Israeli linazidi kuongeza hali ya tahadhari. Biden ametuma meli za kivita na manowari katika Mashariki ya Kati kwa ajili ya maandalizi ya kukabiliana na Iran, na pia ameidhinisha mabilioni ya dola katika mauzo ya silaha ili kuunga mkono kile anacho amini kama "uwezo wa Israeli kukabiliana na vitisho vya adui wa sasa na wa baadaye."

Lakini kuzidi huko kuipatia Israeli silaha haioneshi kuwa kuna uwezekano wa kupunguza vitisho vya kutoka kwa Iran na washirika wake.

Wakati huo huo, kwa matarajio ya kuepusha aina yoyote ya kulipiza kisasi, Biden amesisitiza tena msukumo wake wa kusitisha mapigano Gaza, ambayo Iran imesema inaweza kuchelewesha hatua zake za ulipizaji wa kisasi.

Hata hivyo, Israeli imekuwa ikihujumu mara kwa mara mchakato wa kusitisha mapigano Gaza.

Na ujumbe kutoka Tehran umekuwa mkubwa na wazi: hautakubali shinikizo la Magharibi.

"Madai kama hayo (ya kuepuka kulipiza kisasi) hayana mantiki ya kisiasa, ni kinyume kabisa na kanuni na sheria za kimataifa, na yanawakilisha ombi la kupita kiasi," msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanani alisema wiki hii.

Kwa hivyo Washington iko tayari kuchukua jukumu la kuongezeka kwa mgogoro kati ya Israeli na Irani katika Mashariki ya Kati?

Uhusiano usio na mwsiho

Kwa Tehran, shambulio dhidi ya Israeli ni muhimu kwa sababu mauaji ya Haniyeh yalifanyika kwenye ardhi yake. Wakati huo huo Israeli inaweza kuhalalisha majibu yake kwa shambulio hili linaloweza kutokea kama kujihami na kujitetea.

Mashambulizi na ulipizaji kisasi yanaweza kuzidisha mzunguko wa uchochezi ambao unaivuta Washington zaidi katika vita vya kikanda vinavyoongezeka.

Marekani inasema haitaki hili kutokea. Baada ya Israeli kuwaua majenerali wawili wa Iran nchini Syria mwezi Aprili, Marekani iliishinikiza Israeli kujiepusha na mashambulio dhidi ya Hezbollah - mshirika mkuu wa Iran - na kuamini kuwa Israeli haitashinda katika makabiliano ya muda mrefu.

Kwa hakika, mzozo wa pande nyingi kati ya Israeli na washirika wa Iran, hasa Hezbollah, unaweza kupima kikomo cha msaada usio na masharti wa Marekani kwa Israeli na diplomasia ya mgogoro katika eneo hilo.

Fikiria hali ya utata ya mashambulizi ya Irani na wakati wa shambulio hilo pia. Wanamgambo wa Irani wanaweza kushiriki katika shambulio lolote la Tehran, na kuifanya iwe vigumu kwa Washington kutabiri na kuzuia mashambulizi yanayoweza kutokea kutoka Lebanon, Iran, Syria, Iraq au Yemen dhidi ya Israeli.

Pia kuna gharama za kidiplomasia. Utawala wa Biden unaitilia umuhimu wake kutafuta suluhu la "haraka" la kidiplomasia kati ya Israeli na Hezbollah, na inazingatia mpango huo kama muhimu ili kuepusha vita vikubwa zaidi vya kikanda.

Hata hivyo, kuna hatari ya kupoteza tija ya diplomasia iliyopatikana kwa bidii ikiwa Israeli itafanya matambulizi dhidi ya Iran, au kufanya "mipango ya vita kwa siku za usoni" ili kuhalalisha mashambulizi ya kukera ya "popote na katika eneo lolote."

Kuumiza hisia za umma

Jambo lingine la kuzingatia ni hisia za umma. Wamerakani wana hamu ndogo sana k kwa Amerika kujihusisha katika vita vingine. Kura za maoni zinaonyesha Wamarekani wengi wanapinga kutuma wanajeshi wa Marekani kuilinda Israeli. Uungwaji mkono wa umma kwa hatua hiyo umepungua kwa kasi tangu mashambulizi ya Israeli dhidi ya Gaza kuanza mwaka jana.

Kwa hivyo, ongezeko lolote la mgogoro kati ya Iran-Israeli linaweza kuongeza hatari Washington wakati wa kuzingatia kama kushiriki katika vita visivyopendwa na hatari ya kutenganisha idadi kubwa ya wapiga kura vijana kabla ya uchaguzi wa urais hapo Novemba.

Dola za walipa kodi ni kikwazo cha ziada. Bunge la Marekani na raia wa nchi hiyo wamekuwa wakitofautiana zaidi juu ya matumizi ya Washington katika "vita visivyoisha" - hasa uvamizi wa miaka mingi wa Marekani nchini Afghanistan na Iraq ambao umezaa manufaa kidogo.

Kuongezeka kwa migogoro kati ya Marekani na Irani kunaweza kusababisha Washington kutumia fedha zake za kijeshi kwa Israeli na kutumia pesa za walipa kodi zilizopatikana kwa bidii kupigana vita vingine.

Vita vya Israeli dhidi ya Gaza vimesababisha maelfu ya Wamarekani kupinga ufadhili wa Marekani kwa vita hivyo, huku wengi wao wakikataa kulipa kodi. Sababu zote hizi zinaweza kuifanya iwe ngumu kwa Washington iwapo kutaongezeka kwa mgogoro kati ya Israeli na Irani.

Kuhatarisha wanajeshi wa Marekani

Kuongezeka kwa mgogoro kati ya Iran na Israeli kunaweza pia kuhatarisha mali na vifaa vya jeshi la Marekani katika eneo hilo. Hii inajumuisha idadi kubwa ya wanajeshi wa Marekani walioko katika kambi ndogo za kijeshi katika eneo hilo.

Kuongezeka kwa mgogoro katika eneo hilo na kuongezeka kwa vita vya miezi 10 vya Israeli kunaweza kuongeza nguvu kubwa katika mashambulizi ya siku zijazo.

Baada ya yote, wanamgambo wanaofungamana na Iran walishambulia vikosi vya Marekani mara kadhaa nchini Iraq katika miezi ya mwanzo ya vita vya Israeli dhidi ya Gaza.

Kupanuka kwa vita vya Israeli na Iran kunaweza kuashiria kuingia kwa wahusika wenye nguvu zaidi, kama vile Hizbullah, na kuibua maswali mazito kuhusu maslahi ya kimkakati ya Washington katika Mashariki ya Kati.

Je, inaweza kuizuia Israeli kushambulia Hezbollah, kundi lile lile ambalo Marekani inataka kujihusisha nao kidiplomasia? Na nini maslahi ya Washington katika vita vikali vya Israeli dhidi ya Gaza na kwingineko?

Chaguo mbadala

Badala ya kuendelea kuipatia Israeli silaha kwa ukarimu, idara ya Biden inaweza kuchagua kujibu kwa haraka. Inaweza kutumia mauzo ya silaha kama njia ya kushinikiza Israeli kusitisha mapigano.

Bendera za Israeli na Amerika zikionekana wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin na Waziri Mkuu wa Israeli wa wakati huo Naftali Bennett huko Washington, Jumatano, Agosti 25, 2021.

Kwa miezi kadhaa, mabilioni ya dola wa usaidizi wa kijeshi usio na kikomo yameimarisha mitazamo ya Israeli dhidi ya usitishaji wa vita huko Gaza, na kuchochea upungufu mkubwa wa uaminifu kati ya Israeli na Hamas. Sasa, upungufu huo wa uaminifu unahatarisha kusimamisha juhudi za upatanishi wa hali ya juu huko Doha.

Kwa hivyo, kusitisha usambazaji wa silaha za Israeli kunaweza kutuma ishara kali kwa uongozi wa Waziri Mkuu wa mrengo wa kulia Benjamin Netanyahu kwamba Marekani sasa inataka vita vikali viishe kwa masharti yake yenyewe.

Marekani inapaswa pia kutoa adhabu za muda mrefu kwa Israeli kwa ukiukaji wake wa utaratibu wa sheria za kimataifa, na mateso yaliyofanywa na vitengo vya kijeshi huko Gaza.

Haya yote ni ukiukaji mkubwa wa 'Sheria ya Leahy', ambayo inaitaka Marekani kwa mujibu wa sheria kukomesha usaidizi kwa vitengo vya kijeshi vinavyohusika katika ukiukaji wa haki.

Muda unaisha

Muda unaisha. Washington ilijiunga na Misri na Qatar kwa duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano wiki hii ili kumaliza vita huko Gaza, matokeo ambayo Biden anadai yanaweza kuzuia shambulio la Irani dhidi ya Israeli.

Lakini matumaini mengi juu ya usitishaji vita unaosimamiwa na Marekani yamezidiwa. Tehran imekataa kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja ya kusitisha mapigano, na maafisa wa karibu wa Hezbollah walithibitisha kwa Reuters kwamba kisasi cha Irani kilikuwa kinakuja.

Hili ni muhimu kwa sababu Washington inatafuta njia zaidi za mawasiliano na Tehran kupunguza au kuzuia shambulio la Iran kwa gharama yoyote. Lakini inategemea mchakato wa kusitisha mapigano ambao hauna uaminifu na umetumiwa na Israeli kutekeleza mauaji na upatanishi usiokuwa na tija.

Leo hii, Marekani kushindwa kudhibiti mshirika wake mkuu Israeli inaweka maslahi yake kwenye hatari. Tishio la vita pana zaidi la kieneo linadhoofisha diplomasia ya mgogoro wa Washington, hatari ya uharibifu wa muda mrefu kwa mali ya kijeshi ya Marekani katika eneo hilo, na imeacha uwezo mdogo wa kuzuia mashambulizi ya Iran dhidi ya Israeli.

Washington ina lawama kwa kuongezka kwa mgogoro ambao intaka kuepuka.

Mwandishi, Hannan Hussain ni mtaalamu na mwandishi wa masuala ya kimataifa. Alikuwa anashiriki katika programu ya 'Fulbright Scholar of international security katika chuo kikuu cha University of Maryland ' na amekuwa mashauri wa taasisi ya New Lines Institute for Strategy and Policy huko Washington. Kazi ya Hussain imechapishwa na Carnegie Endowment for International Peace, Georgetown Journal of International Affairs, na Express Tribune (mshirika wa International New York Times).

Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.

TRT World