Timu zilifanya operesheni ya utafutaji na uokoaji baada ya Israel kushambulia kwa mabomu kwenye kambi ya Wapalestina waliokimbia makazi yao katika eneo la Al-Mawasi la Khan Younis, Gaza mnamo Septemba 10, 2024. / Picha: AA

Jumanne, Septemba 10, 2024

2225 GMT - Israeli imewaua Wapalestina 40 na kuwajeruhi wengine 60 katika mashambulizi ya anga kwenye kambi ya hema huko Khan Younis kusini mwa Gaza, madaktari walisema.

Afisa wa ulinzi wa raia wa Gaza ameliambia shirika la habari la AFP mapema Jumanne kwamba "mashahidi 40 na majeruhi 60 walipatikana na kuhamishiwa" katika hospitali za karibu kufuatia shambulio la Israel ndani ya eneo la kibinadamu la Al-Mawasi huko Khan Younis, mji mkuu wa kusini mwa eneo la Wapalestina.

Wakaazi na madaktari walisema kambi hiyo ya hema ilipigwa na angalau makombora manne ya Israeli. Kambi hiyo imejaa Wapalestina waliokimbia makazi yao ambao wamekimbia kutoka mahali pengine kwenye eneo hilo.

Huduma ya dharura ya raia wa Gaza ilisema takriban mahema 20 yaliteketea kwa moto, na makombora yalisababisha mashimo yenye kina cha futi 30.

"Timu zetu bado zinawahamisha mashahidi na waliojeruhiwa kutoka eneo lililolengwa. Inaonekana kama mauaji mapya ya Israel," afisa wa dharura wa kiraia wa Gaza alisema.

Bila kutoa uthibitisho wowote, jeshi la Israel lilisema liliwashambulia wapiganaji wa Hamas ambao ilisema "walikuwa wamejikita ndani ya Eneo la Kibinadamu huko Khan Younis."

Kundi la upinzani la Palestina Hamas lilikanusha kuwa wapiganaji wake walikuwepo katika eneo la mauaji ya Israel, likisema "Madai ya uvamizi wa [Israeli] ya kuwepo kwa wapiganaji wa upinzani ni uongo mtupu."

2152 GMT - Israeli inadaiwa kuwa iliua mateka mnamo Desemba, ilificha ukweli

Jeshi la Israel liliwaua mateka watatu, wakiwemo wanajeshi wawili, wakati wa uvamizi wa Gaza mwezi Disemba na kuficha kwa umma, vyombo vya habari vya Israel viliripoti.

Channel 12 ya Israel imesema mateka watatu wa Israel - Nik Beizer, Ron Sherman na Elia Toledano - waliuawa katika shambulio la anga la Israel lililomlenga kiongozi mkuu wa kijeshi wa kundi la muqawama la Palestina Hamas kaskazini mwa Gaza.

Kwa mujibu wa idhaa hiyo, jeshi la Israel halikujua kuwa kuna mateka wa Israel waliokuwepo pamoja na kiongozi wa Hamas lakini limefahamu undani wa vifo vyao tangu mwezi Februari lakini lilichagua kutovitangaza.

1930 GMT - Pendekezo la Umoja wa Mataifa la Palestina linaitaka Israeli kuondoka Gaza na Ukingo wa Magharibi ndani ya miezi 6

Palestina imesambaza rasimu ya azimio la Umoja wa Mataifa inayoitaka Israel ikomeshe "uwepo wake kinyume cha sheria" katika Gaza iliyozingirwa na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu ndani ya miezi sita.

Mwanadiplomasia wa baraza hilo alisema Wapalestina wanalenga kupiga kura kabla ya viongozi wa dunia wa Baraza Kuu kuanza mikutano yao ya ngazi ya juu ya kila mwaka Septemba 22.

Pendekezo hilo linaitaka Israel kufuata sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuondoa mara moja vikosi vyote vya kijeshi katika maeneo ya Wapalestina.

Rasimu ya azimio hilo sio tu kwamba inadai kukomeshwa kwa shughuli zote za makazi mapya bali pia kuwahamisha walowezi wote wa Kizayuni na kuvunjwa kwa kizuizi cha kujitenga kilichojengwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Inatoa wito kwa Wapalestina wote waliokimbia makazi yao wakati wa kukaliwa kwa mabavu na Israel kuruhusiwa "kurejea katika makazi yao ya asili" na kwamba Israel ilipe fidia "kwa uharibifu uliosababishwa" kwa watu wote katika maeneo hayo.

TRT World