Mabuldoza yalitumika wakati wa operesheni ya jeshi la Israel katika kambi ya Tulkarem na Balata. / Picha: AA

Jumatatu, Septemba 9, 2024

0125 GMT - Jeshi la Israel limevamia mji wa Tulkarem na kambi ya wakimbizi ya Balata katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Vikosi vinavyokalia kwa mabavu vya Israel vilivamia Tulkarem baada ya saa sita usiku, kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Palestina Wafa.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa magari kadhaa ya kijeshi yaliyokuwa yakiandamana na tingatinga mbili nzito yaliingia mjini humo kutoka upande wake wa magharibi, ambapo yalianza kubomoa miundombinu katika eneo la Al-Alemi, huku ndege isiyo na rubani ikipepea juu ya mji huo.

Wafa pia iliripoti kuwa jeshi la Israel lilivamia kambi ya wakimbizi ya Balata mashariki mwa Nablus likiandamana na tingatinga la kijeshi, hali iliyosababisha mapigano na vikosi vya upinzani vya Palestina.

Walioshuhudia walisema kuwa mapigano yalizuka kati ya Wapalestina na jeshi kwenye mlango wa kambi hiyo.

Wanaharakati walishiriki video zinazoonyesha magari ya kijeshi na tingatinga wakati wa uvamizi huo.

0136 GMT - Baraza la mawaziri la usalama la Israeli lakutana kushughulikia mvutano wa Ukingo wa Magharibi

Baraza la mawaziri la usalama la Israel, likiongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, lilikutana kujadili masuala kadhaa muhimu, hasa kuongezeka kwa migogoro katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, mamlaka rasmi ya utangazaji ya nchi hiyo imesema.

Mamlaka hiyo imebainisha kuwa Netanyahu alifungua kikao hicho, ambapo mada kadhaa zilishughulikiwa, zikilenga kushadidi hali katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Wakati vita dhidi ya Gaza vikiendelea, jeshi la Israel limepanua operesheni zake na walowezi wameongeza mashambulizi yao katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, na kusababisha vifo vya Wapalestina 692 na kujeruhiwa wengine karibu 5,700, pamoja na wale waliokamatwa, kwa mujibu wa vyanzo rasmi.

Katika mkutano huo, Netanyahu pia aligusia ziara za mara kwa mara za mawaziri wa serikali katika Msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem.

0104 GMT - Walowezi haramu wa Israel wampiga vibaya Mpalestina mzee baada ya kumteka nyara katika Ukingo wa Magharibi

Walowezi haramu wa Israel walimpiga mzee Mpalestina baada ya kumteka nyara kwa saa kadhaa na kumwachilia karibu na kituo cha ukaguzi cha Meitar kusini mwa Hebron katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Mohammad Abu Sharikh, mtoto wa Hussein Abu Sharikh mwenye umri wa miaka 69, alimwambia Anadolu kwamba baba yake alitekwa nyara mashariki mwa mji wa ad-Dhahiriya katika kijiji cha Khallet al-Tayaran, ambapo alikuwa akichunga kondoo wake.

“Walowezi watano wenye silaha wakiwa wameandamana na askari walimteka babangu mwendo wa saa 12:30. (1530GMT) na kumpeleka kwenye makazi ya Tina, ambapo alikaa kwa saa nne na alipigwa wakati huo, "akaongeza mwana huyo.

TRT World