Hatua hiyo, pia itawezesha upatikanaji wa kirahisi wa misaada ya kibinadamu katika eneo la Palestina./Picha: AA  

Kikundi cha Palestina cha Hamas na Israeli zimefikia makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza na pia kukubaliana ubadilishanaji wa wafungwa, kulingana na Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Qatar.

Msuluhishi huyo wa mgogoro huo, alisema siku ya Jumatano kuwa awamu ya 42 ya kusitisha mapigano hayo itafanyika Januari 19.

Maafikiano hayo yanafuatia wiki kadhaa za usuluhishi zilizofanyika nchini Qatar, ambapo zilihusisha mpango wa kuwaachilia mateka wa Israeli kwa awamu pamoja na kuwaachilia mamia ya wafungwa wa Kipalestina kutoka magereza ya Israeli.

Mpango huo, pia utahusisha kurudi nyumbani kwa wakazi wa Gaza waliokimbia makazi yao.

Hatua hiyo, pia itawezesha upatikanaji wa kirahisi wa misaada ya kibinadamu katika eneo la Palestina.

Hadi kufikia sasa, Israeli inawashikilia zaidi ya wafungwa 11,000 wa Kipalestina, huku ikikadiriwa kuwepo na idadi ya Waisraeli 98 ndani ya Gaza.

Kwa kipindi kifupi, Israeli ilisitisha mapigano hayo kwa muda wa siku sita ndani ya mwezi Novemba 2023, hatua iliyowezesha kuachiwa kwa mateka 50 wa Kiisraeli waliokuwa wanashikiliwa Gaza na wafungwa 150 wa Kipalestina ndani ya Israeli.

Hata hivyo, sitisho hilo halikudumu kwa muda mrefu huku Israeli ikiendeleza mashambulizi yake katika eneo hilo.

Hatua hiyo ililaumiwa na watu wa ndani wa Israeli, ambao walinyooshea Waziri Mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu kidole cha lawama.

Makundi ya wanasiasa na viongozi wa kijeshi wanasema kuwa hatua ya Netanyahu inalenga kuendeleza vita ili kuimarisha nafasi yake kisiasa.

Kulingana maofisa wa afya wa Palestina, mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 46,700 katika eneo hilo.

Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati ya kuwakamata Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na Waziri Mkuu wa zamani wa ulinzi wa nchi hiyo kwa kusababisha uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.

Hali kadhalika, Israeli inakabiliwa kesi ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

TRT Afrika