Ni kawaida kwa wengi kuichukulia Marekani kama kiongozi wa kiuchumi duniani.
Nchi ambayo inatazamiwa kuwa ndoto ya wengi kufikia, kutokana na uwepo wa rasli mali zake na fursa nyingi za kujiendeleza.
Lakini ukitumia darubini utaona undani wake. Matatizo yaliyopakwa rangi juu.
Marekani imo katika deni. Inadaiwa kila upande kiasi kuwa haiwezi kumudu gharama za kuendesha serikali bila kukopa. Tatizo ni kuwa, bunge la Congress limekuwa katika mvutano na serikali ya Joe Biden kuhusu kuruhusu serikali kupandisha kiwango cha kukopa.
Wanachama wa Democrats walidai kuongezewa pesa ila Republicans wanadai kwa hilo kufanyika lazima waweke masharti makali ambayo kwa mtazamo wa Democrats yanawafaidisha wao.
Kuogopa siku ya 'adhabu'
Ukweli ni kuwa tangu mwaka wa 2001, Marekani imeshindwa kukusaya fedha ya kutosha kukidhi mahitaji yake.
Isitoshe, ni katika muda huu ambapo Marekani imeona kuongezeka mara dufu kwa matumizi yake kupita kiasi, ama kutokana na oparesheni za kijeshi na gharama za vita, au uwekezaji wa teknolojia mpya. Nchi hiyo imelazimika kukopa zaidi kila mwaka.
Hiki kiwango cha mwisho cha kukopa nchini Marekani ndicho kinajulikana kama kiwango cha ukomo au ‘Debt Ceiling.’
Hiki kiwango kisipo idhinishwa na Congress kupandishwa, na kuruhusu nchi hiyo kukopa zaidi, basi serikali inashindwa hata kulipa madeni yake ya ndani ya nchi na ya nje.
Mzozo uliopo sasa ni kuwa tarehe ya mwisho ya Marekani kuidhinishwa kukopa itafikia Juni mosi. Mwanzoni kulikuwa na Imani kuwa wanaweweza kubambanya matumzii hadi mwezi Agosti, lakini baada ya kufanya hesabu zake, wakagundua kuwa hawana fedha za kukimu mahitaji zaidi ya Juni.
Marekani inakopa wapi madeni yake?
Kwa kuwa inatazamiwa kuwa nchi tajiri duniani, ni vigumu kuamini Marekani pia inaweza kukopa deni kwingine.
Lakini inakopa, na la kushangaza ni kuwa taifa lile ambalo Marekani inakinzana nayo ndio mkombozi wake kiuchumi, China.
‘‘Sasa hivi tishio kubwa kwa Marekani sio Urusi bali ni China,’’ anasema Dkt Anthony Francis Mveyange, mchumi wa maendeleo nchini Kenya. ‘‘Nayo Marekani itafanya juu chini kuhakikisha haishindwi kulipa madeni yake kwa China.’’ Ameongeza.
Tangu 2011, dari la deni la Marekani limekuwa likipanda kutoka $11.9 Bilioni hadi kima cha sasa cha $31.4 Trilioni.
Hata hivyo kwa kuwa taifa halikuwa likikusanya fedha za kutosha kukidhi matumizi yake, ililazimika kukopa zaidi ya sehemu moja. Baadhi ya wadeni wake wakubwa ni:
• Japan – $1.1 Trilioni
• China - $859 Bilioni
• Uingereza - $668 Bilioni
Jumla ya madeni ya Marekani ya nje ni 31 % . Lakini Marekani pia inakopa ndani ya nchi, ikiwa ni jumla ya 69%, ya deni lake, kutoka kwa biashara za wenyeji, mabenki, hazina ya kustaafu na wananchi wengine.
Wataalamu wa kiuchumi wanasema kuwa, mkasa wa deni la Marekani sio kama mwingine wowote tulio ona. ‘‘Marekani haiwezi tu kukosa kulipa madeni yake kama vile walivyofanya Ugiriki, Argentina au Zambia. Ni kwasababu, huu mkasa wa Marekani haukutokana na kudorora kwa uchumi bali ni mkasa wa kutengenezwa na watu.’’ Amesema Dakt Francis Mveyange.
Basi nini kinaweza kutokea Marekani ikikosa kulipa deni lake?
Hali mbaya zaidi ni pale rais anapokosa kuafikiana na Bunge la Congress juu ya kuongeza mkopo wake kabla ya siku ya mwisho ya kulipa deni, ambayo mwaka huu ilikuwa Juni Mosi. Marekani ingekumbwa na mkasa mkubwa sana.
Bado hakujatokea kitu kama hiki, japo mara kadhaa imetishiwa kama ilivyotishiwa mwaka huu. Dakt. Francis Mveyange anasema kuwa athari la karibu zaidi ni watu kupoteza Imani na Marekani kama mkopaji. ‘‘Ni kama vile deni lako binafsi, ukikosa kulipa kwa wakati, hakuna mtu atakaye kukopesha tena kwani hawaamini utalipa kikamilifu au utalipa kwa wakati.’’
Dakt Mveyange anaongeza kuwa wakikosa kulipa, basi itawalazimu wadeni wao kurejelea masharti ya kuwakopesha siku zijazo, kwa maana kuwa watazidisha riba wanayotoza kama njia ya kujikinga. Tumeone hili likifanyika kwa mataifa ya Afrika.’’
Kwa serikali inayotegemea zaidi madeni kuendesha shughuli zake za kila siku, watakuwa na wakati mgumu sana.
Huduma za serikali zitasita. Mishahara itakosa kulipwa, malipo ya uzeeni itasitishwa. Uzalishaji wa ndani utakoma.
Makampuni yatalazimika kuwasimamisha wafanyakazi wao. Ukosefu wa ajira utasababisha kudorora kwa uchumi.
Mabenki mengi yanakopesha seikali pesa kupitia hisa na mafungo ya benki kuu. Pale habari inatoka kuwa serikali imeshindwa kulipa deni lake,basi wasiwasi huenea na kusababisha watu kukimbili amabenki kutoa hela yao waliohifadhi huko.
Hii ndio inaitwa 'Bank Rush' ambayo husababisha mabenki kuporomoka na kuanguka kwa bei za hisa.
Usaliti
Mchambuzi Dakt Francis Mveyange anasema kuwa mvutano kati ya viongozi wa Democrat na Republican nchini Marekani umekuwepo kwa miaka mingi.
‘‘Tuliona 2011 wakati wa utawala wa Obama.Viongozi wa Republicans walitaka kukwamisha shughuli za serikali na wanatumia mkopo huu kama kigezo chao.’’
Pande zote mbili, zinaweza kulaumiwa juu ya hu mkasa waliojiundia.
Wakati wa majadiliano katika bunge la Congress na seneti wengi wao wanataka kulazimisha masharti yanayowafaidi wao kulimgana na upande upi upo serikalini.
Haina maana kuwa hili likitokea rais anakuwa hana namna kabisa, la. Rais akibanwa zaidi anao uwezo wa kutumia sharia ya kumi nan nne ya katiba ya Marekani, ambayo kimsingi inampa rais uwezo wa kulivuka bunge katika mamauzi ya dharura ya serikali.
Lakini wachambuzi wanasema kuwa hili litasababisha tu mvutano mahakamani kuotokana na vyama kukata rufaa.
Dkt. Francis Mveyange anasema, ‘‘Kwa sasa utawala wa Biden unaweka matumaini kwa kuwa wafanya biashara wakubwa nchini Marekani ni wa Republican kwa hivyo hawawezi kukubali kuona uchumi ukiporomoka.
Kimsingi wachambuzi wanasema kuwa serikali ya Marekani haiwezi kukubali kutumbukia katika mkasa wa kifedha na kukosa kulipa madeni yake kwani itasababisha kupoteza heshima yao kimataifa
'’Kiburi chao hakiwezi kuruhusu uchumi kuporomoka, kwani wanajua watapoteza hadhi yao kimataifa, kama kiongozi wa uchumi duniani.’’ Dkt Mveyange anaongeza, ‘wakiruhusu hili kufanyika, raia wa Marekani hawata wasamehe.’’