Ripoti zilidai kuwa Israel imeshambulia hospitali ya Urafiki ya Uturuki na Palestina ya Gaza, hospitali pekee ya saratani katika eneo lililozingirwa, Jumatatu. / Picha: AA

Kitengo cha serikali ya Uturuki cha kupambana na habari za kupotosha kimechukua hatua kukanusha madai kwenye mitandao ya kijamii kwamba Israel ililenga maghala ya Red Crescent ya Uturuki na kuharibu jengo linalomilikiwa na Urais wa Usimamizi wa Majanga na Dharura wa Uturuki (AFAD).

Kituo cha Kupambana na habari potofu kilitoa taarifa siku ya Jumatatu katika mtandao wa X kikisema jengo linalozungumziwa, ambalo liliripotiwa kuharibiwa sana na mashambulizi ya Israel, lilikuwa ni ghala la misaada ya kibinadamu linalomilikiwa na 'Red Crescent' ya Palestina ambalo lilijengwa kwa msaada wa 'Red Crescent' ya Uturuki.

"Madai kwamba 'Israel ililenga maghala ya Hilali Nyekundu ya Uturuki na kusababisha uharibifu mkubwa kwa jengo la AFAD' kwenye akaunti fulani za mitandao ya kijamii si ya kweli. Shirika la Hilali Nyekundu la Uturuki lilisaidia katika ujenzi wa kituo cha Hilali Nyekundu ya Palestina na haina vifaa vya wala oparesheni huko Gaza. Tafadhali puuza madai yasiyo na msingi,” ilisema taarifa hiyo.

Tangu mwishoni mwa juma, jeshi la Israel limepanua mashambulizi yake ya angani na ardhini kwenye Ukanda wa Gaza, ambao umekuwa chini ya mashambulizi ya angani tangu mashambulizi ya kushtukiza ya kundi la muqawama la Palestina Hamas tarehe 7 Oktoba.

Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi ya Israel huko Gaza imepanda hadi 8,306, Wizara ya Afya katika eneo lililozingirwa ilisema Jumatatu.

"Waliofariki ni pamoja na watoto 3,457 na wanawake 2,136, huku zaidi ya watu 21,048 wakijeruhiwa," msemaji wa wizara hiyo Ashraf al Qudra aliuambia mkutano wa waandishi wa habari huko Gaza.

Takriban Waisrael 1,538 wameuawa katika mzozo huo.

TRT World