Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, katika hotuba yake kwa taifa kufuatia matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2023, alisifu ushindi wake kama ushindi wa demokrasia.
Akizungumza mbele ya mamia ya maelfu ya watu waliokusanyika katika ua wa jengo la rais mjini Ankara, Rais Erdogan alisisitiza umoja, na kutangaza kwamba washindi wa kweli wa duru ya pili ya uchaguzi wa Jumapili walikuwa raia milioni 85 wa Uturuki na demokrasia ya Uturuki.
“Uturuki ndiye mshindi, demokrasia yetu ndio mshindi, Hakuna aliyepoteza leo. Sisi wote milioni 85 tumeshinda. Sasa ni wakati wa kuungana kutimiza malengo yetu ya kitaifa na ndoto za kitaifa” Erdogan alisema.
Kuchaguliwa tena kwa Erdogan kulithibitishwa na mwenyekiti wa Baraza Kuu la Uchaguzi nchini humo (YSK) Jumapili jioni.
Kwa mujibu wa matokeo yasiyo rasmi, Ahmet Yener alisema Erdogan alishinda kwa asilimia 52.14, huku Kilicdaroglu akipata asilimia 47.86 ya kura, na kuongeza kuwa asilimia 99.43 ya masanduku ya kura yamefunguliwa hadi sasa.
"Karne ya Uturuki" "
Katika moja ya chaguzi muhimu zaidi katika historia ya vyama vingi vya siasa, taifa letu lilifanya uamuzi wake kwa ajili ya 'Karne ya Uturuki'," Erdogan alisema. Aliongeza kuwa uchaguzi huu ulikuwa "muhimu zaidi" kwa Uturuki katika zama za kisasa.
"Tunapaswa kufanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya watu wetu,ili Kuponya majeraha ya tetemeko la ardhi la Februari 6 na kujenga upya miji iliyoharibiwa kutaendelea kuwa kipaumbele cha juu cha serikali " Erdogan alisema.
Pia aliwakumbusha watu kwamba siku iliyofuata, Mei 29, inalingana na kumbukumbu ya kutekwa kwa Istanbul na Sultan Mehmet II wa Ottoman mnamo 1453.
"Ushindi wa Istanbul, ambao tutaadhimisha kesho katika kuadhimisha miaka 570, uliashiria mwanzo wa enzi mpya huku ukimaliza enzi ya zamani," Erdogan alisema.
"Natumai wakati huu muhimu katika historia yetu ya Karne ya Uturuki ambayo tunaona chaguzi kama hizi itaacha alama yake." Erdogan
Pia alivikosoa vyombo vya habari vya mataifa ya Kigeni kwa propaganda zao dhidi ya azma yake ya kuchaguliwa tena. "Vyombo vya habari vya Magharibi vimepoteza," alisema, akiongeza kwamba walichapisha taarifa tata ili "kumuangamiza".
Kurudi kwa wakimbizi wa Syria makwao
Zaidi ya Wasyria milioni 3.7 kwa sasa wanaishi Uturuki.
"Hadi sasa, tumewezesha kurejea kwa hiari kwa karibu watu 600,000 katika maeneo salama katika nchi ya Syria.Kupitia mradi mpya wa makazi mapya tunaoufanya na Qatar, tutahakikisha kurejea kwa watu milioni 1 zaidi katika miaka michache ijayo." Alisema Erdogan Kuhusu kurejea kwa hiari kwa wakimbizi wa Syria.
Kufuatia kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria mwaka 2011, Uturuki alipitisha sera ya "mlango wazi" kwa Wasyria wanaokimbia mateso na ukatili.
Syria imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mapema mwaka 2011, wakati utawala wa Bashar al Assad ulipodhibiti maandamano ya kuunga mkono demokrasia kwa ukatili usiotarajiwa.
Mamia ya maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni 10 kukimbia makazi yao, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.