Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikutana na Elon Musk kabla ya mkutano wa 78 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York./Picha: AA

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa Uturuki itachukua hatua madhubuti za kushirikiana na Elon Musk katika nyanja ya kiteknolojia iwapo fursa kama hizo zitajitokeza, chombo cha TRT Haber kimeripoti.

Siku ya Jumanne, Rais mteule wa Marekani Donald Trump alimteua Musk katika nafasi ya kuongeza ufanisi serikalini, akimpa jukumu hilo mtu tajiri zaidi ulimwenguni aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuchaguliwa kwa Trump.

"Musk ni mfanyabiashara anayefanya kazi kwenye sekta za anga na za teknolojia," alisema Erdogan siku ya Jumatano baada ya kurudi kutola Baku.

"Teknolojia sio nyanja unayoweza kufanikiwa ukiwa mwenyewe, kwa vyovyote vile unahitaji ushirikiano."

Mahusiano ya karibu

Hapo awali, Rais wa Uturuki Erdogan amewahi kukutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Tesla Elon Musk na kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo magari ya kutumia umeme hadi miradi ya anga za mbali.

Mwaka jana, Erdogan alimualika Musk kujenga kiwanda cha kutengeneza magari aina ya Tesla nchini Uturuki baada ya wawili hao kukutana katika Jumba la Uturuki (lijulikanalo kama Kituo cha Turkevi) jijini Manhattan, nchini Marekani.

Erdogan pia alimshirikisha hatua zilizopigwa na Uturuki kupitia maono ya "Uturuki ya Kidijiti" na Mkakati wa Kitaifa wa Akili Mnemba.

Musk alimwambia Erdogan kuwa wasambazaji wa Uturuki walikuwa wanafanya kazi Tesla na kwamba Uturuki ni kati ya maeneo sahihi kwa kiwanda kingine.

Akijibu pendekezo la Rais Erdogan la ushirikiano na huduma za satelaiti ya SpaceX’s Starlink, Musk alisema kuwa alitamani kushirikiana na mamlaka za Uturuki ili kupata leseni ya kutoa huduma za Starlink nchini Uturuki.

Musk aliitembelea Uturuki Novemba mwaka 2017, ziara ambayo ilifungua milango ya ushirikiano kwenye kutumia teknolojia za kurusha roketi za kampuni hiyo.

Hivi karibuni, Uturuki ilizindua satelaiti yake ya kizazi cha tano ya Turksat 5A kwa kutumia roketi ya SpaceX ya Falcon 9 kutoka kituo cha kampuni cha Cape Canaveral huko Florida.

TRT Afrika