Mnamo 1978, Tanzania haikusafiri kuchuana na Uganda kufuatia mvutano wa kisiasa kati ya mataifa hayo mawili. Uganda ilitinga fainali hizo baada ya kupewa walkover kwa mechi ya kufuzu kwa makala ya 11 ya Afcon nchini Ghana na kumaliza Afcon ya mwaka huo baada ya kujiandikishia matokeo yenye mafanikio zaidi kwa kufika fainali.
Tanzania ilifuzu AFCON 2019 baada ya kuizaba Uganda 3-0 kwenye mchuano uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, mnamo Machi 24, 2019.
Lakini 2021, ilikuwa ni majonzi na machozi kwa mashabiki wa timu hizo za Uganda na Tanzania kwani mataifa hayo hayakufuzu kwa makala ya AFCON 2021.
Hata hivyo, mambo yamechemka leo, namna wanavyopenda kusema, kwani lazima mmoja atalia ifikapo mwisho wa siku baadaye leo.
Cha kustajaabisha mno kati ya Tanzania na Uganda, ni kuwa kila mmoja alimnyuka mwenzake 1-0 na kuifanya ainisho la Head-to-head kuwa ngumu mno.
Aidha, Niger imeziharibia timu zote mbili hesabu kwa kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania kabla ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Uganda.
Hadi kufikia hapa, jumla ya mataifa 15 tayari yamejihakikishia nafasi ya kushiriki Afcon 2023, ikiwa pamoja ve wenyeji Côte d'Ivoire, waliofuzu moja kwa moja kwa wenyeji.
Hii inamaanisha kuwa ni Tanzania au Uganda itakayobahatika kujaza mojawapo ya nafasi 9 pekee zilizosalia kunyakuliwa, katika mechi za mwisho za kutinga Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka ujao.
Taifa Stars itasafiri hadi Annaba kukutana na viongozi wa Kundi F, Algeria, ambao tayari wamejihakikishia nafasi nchini Côte d'Ivoire, huku Uganda ikikutana na Niger kwenye Uwanja wa Stade de Marrakech, Morocco.
Tanzania inashikilia nafasi ya pili kundi F ikiwa na pointi 7 nayo Uganda ina pointi 4 ikishikilia nafasi ya tatu. Uganda Cranes, itasonga hadi pointi saba, na kusajili alama sawa na Tanzania Iwapo itaishinda Niger.
Tanzania, inayolenga kushiriki AFCON kwa mara yake ya tatu katika historia yake, itaingia uwanjani dhidi ya Algeria ikisaka sare au ushindi huku ikilazimika kujiepusha na kufungwa.
Algeria tayari imeifunga Uganda 2-1 na 2-0 pande hizo zilpokutana kwenye mechi za kufuzu huku Algeria pia ikijinyakulia ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
Uganda nayo inaelekea kwenye mchezo wake Marrakech ikihitaji pointi zote tatu dhidi ya Niger. Uganda Cranes ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Niger wakati wawili hao walipokutana awali mnamo Juni 8, 2022 katika uwanja wa Kitende, Kampala.
Kwa upande mwingine, baada ya kukosekana kwa miaka 39, Uganda hatimaye ilirejea katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2017 nchini Gabon.
Hii leo Uganda inasaka tiketi ya kushiriki Afcon kwa mara yake ya nane kuonekana katika michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka barani Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957.
Dimba la Afcon 2023, iliyoahirishwa hadi Januari 2024, litachezwa kuanzia tarehe 13 Januari 2024 hadi tarehe 11 Februari 2024 huku mchuano wa ufunguzi ukiandaliwa katika Uwanja wa Alassane Ouattara, mjini Abidjan, nchini Côte d'Ivoire.