Timu ya taifa ya soka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kudhihirisha ubora wake kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, baada ya kushika nafasi ya kwanza tena kwenye ukanda huo.
DRC, inayonolewa na kocha Sebastien Desabre imepanda nafasi moja katika orodha ya ubora wa FIFA, huku ikivuna alama 1,431.
Uganda iko katika nafasi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikichupa hadi nafasi ya 87 ulimwenguni.
'The Cranes' ilipanda nafasi tatu ulimwenguni baada ya kufanikiwa kujikusanyia alama 1,269 kwenye orodha hiyo iliyotolewa siku ya Oktoba 24, 2024.
Kulingana na orodha ya viwango vya ubora wa soka, Kenya iko katika nafasi ya tatu katika ukanda wa EAC.
Hata hivyo, kikosi cha 'Harambee Stars', kimeporomoka kwa nafasi nne katika orodha hiyo kwa kushika nafasi ya 106 ulimwenguni, ikiwa imejikusanyia alama 1,195.
Majirani zao, Tanzania wako katika nafasi ya nne kwa ubora ndani ya EAC, ikiwa pia katika nafasi ya 112 ulimwenguni, baada ya kupata alama 1,173.
Hata hivyo, 'Taifa Stars' imeporomoka nafasi mbili kwenye orodha hiyo, hasa baada ya kupoteza michezo miwili dhidi ya DRC kwenye hatua ya kufuzu mashindano ya AFCON kwa mwaka 2025.
Nafasi ya tano kwa ubora ndani ya EAC inakwenda kwa timu ya Taifa ya Rwanda, ambayo iko kwenye nafasi ya 126 ulimwenguni, ikiwa imevuna alama 1,130.
'Amavubi' imporomoka kwa nafasi nne kidunia, kulingana na orodha ya FIFA.
Kwa upande wake, “Les Hirondelles” timu ya Taifa ya Burundi ni 139 ulimwenguni, ikishika nafasi ya sita katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Timu hiyo imeporomoka nafasi tatu, na kukusanya alama 1,089.
Sudan Kusini iko katika nafasi ya sita katika ukanda wa EAC, wakati Somalia inashika mkia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande mwingine, timu ya taifa ya Morocco ndiyo ya kwanza kwa ubora barani Afrika, ikishika nafasi ya 13 ulimwenguni.
Simba hao kutoka milima ya Atlas, wamepanda nafasi moja juu katika orodha hiyo, wakijikusanyia alama 1,681.
Nigeria imepanda kwa nafasi tatu katika orodha hiyo, ikishika nafasi ya nne barani Afrika na ya 36 ulimwenguni.