Idadi ya wagonjwa wa kisukari inatarajiwa kuongezeka. / Picha: Getty Images

Dunia ikiadhimisha siku ya kisukari duniani, Shirika la Afya Duniani, WHO inaonya kuwa idadi ya watu wanaopata ugonjwa huo barani huenda ikaongezea iwapo jitihada zaidi hazitachukuliwa kupambana na ugonjwa huo.

Kisukari au 'diabetes' ni ugonjwa sugu ambao hutokea wakati kongosho itaposhindwa kutoa 'insulini' ya kutosha au wakati mwili hauwezi kutumia ipasavyo insulini inayozalisha. Insulini ni homoni inayodhibiti sukari ya damu.

"Bila uingiliaji wa haraka, utabiri ni kwamba idadi ya watu wanaoishi na kisukari Afrika itapanda hadi kufikia milioni 54 ifikapo mwaka wa 2045, ongezeko kubwa zaidi linalotarajiwa ulimwenguni," Dkt. Matshidiso Rebecca Moeti, Mkurugenzi wa WHO Afrika amesema katika taarifa yake.

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa katika Ukanda wa Afrika, zaidi ya watu wazima milioni 24 kwa sasa wanaishi na kisukari, nusu yao wakiwa bado hawajagunduliwa.

"Changamoto zaidi ni kwamba Afrika ina kiwango cha chini cha uwekezaji katika huduma ya kisukari duniani kote, ikiwa ni 1% tu ya matumizi ya afya ya kanda. Mifumo ya afya pia imeundwa kimila ili kukabiliana na magonjwa ya papo hapo, ya kuambukiza, bila uangalifu wa kutosha kwa magonjwa sugu kama kisukari," Moeti ameongezea.

Jitihada za kupambana na Kisukari

Wataalamu wa afya wanasema ugonjwa wa kisukari usipotibiwa unaweza kusababisha matatizo kama vile ugonjwa wa moyo, kiharusi, uharibifu wa mishipa ya fahamu, figo kushindwa kufanya kazi vizuri, kukatwa kiungo cha chini cha mguu, na magonjwa ya macho ambayo yanaweza kusababisha upofu.

WHO inasema kudhibiti ugonjwa wa kisukari kunahitaji juhudi endelevu za kusawazisha shughuli za afya ya kimwili, lishe bora, ustawi wa kiakili.

"Muhimu pia ni mikakati ya kina ya kuzuia kushughulikia mambo ya hatari ikiwa ni pamoja na uzito uliopitiliza, chakula duni na shughuli za kimwili, pamoja na ushirikiano wa jamii ili kuhakikisha mifumo bora ya usaidizi na kupunguza unyanyapaa," Moeti amesema.

Katika kikao cha 78 cha Kamati ya Kanda ya WHO ya Afrika mwezi Agosti mwaka huu, nchi Wanachama wa Afrika ziliidhinisha Mfumo wa WHO wa Utekelezaji wa Mkataba wa Kisukari Duniani (GDC) barani Afrika.

Nia kuu ikiwa ni kulenga zaidi kupambana na changamoto ya kujumuisha huduma za kisukari katika mifumo mipana ya afya, na kutoa muongozo kwa nchi kuimarisha kinga, utambuzi na matunzo ya ugonjwa wa kisukari, hasa katika ngazi ya afya ya msingi.

TRT Afrika