Wabunge wa Kenya wameelezea hofu yao kwa Uganda kuendelea kuwashikilia wafugaji 40 kutoka Kenya wenye asili ya Turkana katika nchi jirani ya Uganda.
Inadaiwa wafugaji walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi nchini Uganda na kufungwa jela , kwa njia ambayo wabunge wa Kenya wanadai ni kinyume na sheria.
Katibu wa wizara ya mambo ya nje , Dkt. Alfred Mutua alifafanua katika taarifa hiyo, kwamba kukamatwa kwa wafugaji hao kumesababishwa na matukio kadhaa kufuatia mauaji ya wanajiolojia watatu wa Uganda na askari wawili wa jeshi la ulinzi la wananchi wa Uganda.
Inadaiwa silaha zao ziliibwa mnamo Machi 2022. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafugaji wanane wa kwanza walikamatwa Machi 2022 na inadaiwa walikana kufanya mauaji hayo.
Hata hivyo, walifungwa jela miaka 20 kila mmoja kwa kupatikana na bunduki kinyume cha sheria.
"Wafugaji wengine 32 walikamatwa wakati wa oparesheni ya msako wa jeshi la Uganda la UPDF huko Turkana mnamo Aprili 8, 2023, na baadaye kufikishwa mahakamani na kufungwa jela miaka 10 kwa madai ya kumiliki bunduki kinyume cha sheria," wazieri aliambia bunge.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekataa wasiachiliwe.