Timu nyingi za soka Afrika zimesheheni nembo na majina ya wanyama. Picha/Reuters. 

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Katika uzinduzi wa Kombe la Mataifa Afrika 2023, Tembo wa Côte d'Ivoire wamewatandika Mbwa mwitu wa Guinea Bissau 'Djurtus' kwa mabao mawili kwa bila.

Kuanzia kwenye karatasi hadi kwenye uzani 'Tembo' mnyama mzito kuliko wote duniani alistahili kushinda kwa haki mnyama huyo mdogo.

Timu nyingi za soka Afrika zimesheheni nembo na majina ya wanyama kwa vile barani humo kunashuhudiwa baadhi ya wanyama wenye sifa kubwa mfano hai ikiwa ni Simba.

Nchi tatu zilichagua kama nembo na jina mnyama Simba 'Mfalme wa wanyama': Simba wa Nyika wa Cameroon, Simba wa [Milima] ya Atlas wa Morroco, Simba wa Teranga [ukarimu] wa Senegal.

Kuanzia kwenye karatasi hadi kwenye uzani 'Tembo' mnyama mzito kuliko wote duniani. Picha/Reuters.

''Jina hili la Simba ni kujenga matumaini na dhana kwamba ndio 'wafalme' wa uwanjani,'' anasema mwandishi mwandamizi wa soka kutoka Burundi Rashid Alfred.

''Kutokana na mbwembwe zake, Simba anaashiria heshima. Lakini pia anakutia hofu'' alisititiza mkongwe Rashid Alfred mwenye umri wa miaka 78.

''Wakati Senegali wanaingia uwanjani, wanapambana kama Simba: Wanajitupa kutafuta mawindo au chakula. Unawaona, wanahisi njaa. Wana nia yao kukuchana na kukutafuna.''

Wanyama wakali

Timu nyingi zimechagua pia majina ya wanyama au wadudu wa kila aina kutokana pengine na wepesi wa kupenya au wa kuruka lakini kila mara wakitilia maanani hasa suala la uwezo na nguvu.

Mfano: Utawala wa Rais Mobutu Sese Seko nchini Zaire ya zamani. Alichagua mnyama 'Chuwi' kama nembo yake ya mamlaka pamoja na Timu ya Taifa,'' alikumbusha mwanamichezo Rashid Alfred.

"Na timu ya DRC ilirejelea jina hilo la Chuwi wa Congo baada ya kuitwa kwa muda mfupi ' Simba."

Mara ya wananyama mara nyingi yanazingatia ni mnyama upi ambae atapata muafaka katika jamii na kumfurahisha kila mmoja. Picha/Sportingnews.        

Kwa upande wake mwanasosiolojia Nicodeme Bugwabari anasema, ''Katika chaguo la nembo au jina, unajaribu kutengeneza dhana kwamba nembo hiyo itapata uungwaji mkono lakini pia kuoana na mtazamo wako na jinsi wewe unavyofikiria. Ni mnyama upi ambae utapata muafaka katika jamii na kumfurahisha kila mmoja. Na kuanzia hapo unasukuma pia ujumbe kwa mpinzani au adui,'' anasema Bugwabari.

Majina ya wanyama yamezidi kuibuka kwa Timu za taifa:

Pengine kwa kuzingatia nguvu ya utulivu kama 'N'gombe wenye Nundu' [Zebus] wa Madagascar, lakini pia nguvu ya kuuma kama 'Nge wa Gambia' au pia nguvu ya kustawi kama 'Farasi' wa Burkina Faso.

Kumekuwepo pia chaguo la majina ya wanyama kutokana na maumbile ya nchi na wingi wa vilivyo hai katika nchi husika nama vile Chuwi wa Gabon 'Pantheres.'

Lakini licha ya vigezo mbalimbali, hata hivyo ''Barani Afrika, kuna wanyama wanaoheshimika zaidi lakini kwa bahati mbaya hamna timu yoyote inayokubali kubatizwa majina yake au kutambulishwa kwa jina lake la utani.

Nchi tatu barani Afrika zilichagua jina la Tai [Eagle] :Tunisia (Tai wa Carthage), Nigeria (Super Eagles) na Mali (Tai wa Mali). Picha/Reuters. 

''Kwa mfano: Kobe. Kila mtu barani Afrika atakwambia ni mnyama mwenye akili sana. Lakini soka yaashiria mapambano na nguvu. Kwa maana hiyo anatafutwa mnyama wenye nguvu ya kushinda. Na sio mnyama mwenye ujanja. Kinachohitajika hapa ni ari, kasi, stamina na nguvu,'' anafafanua Rashid Alfred.

Majina asilia

Nchi tatu barani Afrika zilichagua jina la Tai [Eagle] :Tunisia (Tai wa Carthage), Nigeria (Super Eagles) na Mali (Tai wa Mali).

Baadhi pia ya timu za taifa za soka Afrika zinatumia majina ya lugha za asili lakini wakiashiria wanyama au wadudu. Mfano ni 'Intamba wa Burundi'' au ndege aina ya Mbayuwayu au pia 'Amavubi 'ikimaanisha' Nyuki wa Rwanda,'' lakini vile vile 'Djurtus' wakifahamika kama mbwa mwitu wa Guinea Bissau na kadhalika....

Sheria ya msituni uwanjani ikoje?

Mwaka uliopita, Bénin walibadili rasmi jina la Timu ya Taifa.'' Kindi au'Squirrel' waligeuka na kuitwa Duma 'Cheetahs.'

Kanuni za msitumi hazifanyi kazi katika mpira, mwenye nguvu anaweza kushindwa na asiye na nguvu. Picha/Reuters.

''Jina hilo la awali liliwajengea dhana kwamba wasingeweza kushinda au kufika mbali mashindanoni kutokana na udhaifu wa mnyama.'' alikejeli mwandishi huyo Alfred.

Lakini akakumbusha ile methali ya wahenga kwamba, ''Punda anaweza kubadili jina lakini atabaki kuwa ni punda tu.'' Licha ya kubadili jina, Benin hawakufuzu kwenye makala haya ya 34 ya Kombe linalochezewa nchini Côte d'Ivoire.

Na katika Kombe la Mataifa ya Afrika la mwaka wa 2019 nchini Misri, Simba wa Teranga walitafunwa vibaya na 'Fennecs', mbweha wa jangwani wa Algeria. Kwa maana hiyo, ni wazi kwamba sheria ya msituni mara kwa mara haifanyi kazi katika soka: Aliye dhaifu anaweza pia kumkung'uta mwenye nguvu.

TRT Afrika