Zaidi ya watu 20 wameuawa baada ya makombora kulenga soko katika kitongoji cha mji mkuu wa Sudan Khartoum siku ya Jumapili, kamati ya wanasheria wanaounga mkono demokrasia imesema katika taarifa yake.
Ilikuwa ni umwagaji damu wa hivi punde zaidi katika mapigano tangu Aprili kati ya vikosi vya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza Kikosi cha Kusaidia Haraka (RSF).
Taarifa kutoka kwa kamati ya mawakili wanaounga mkono demokrasia ilisema makombora hayo yaligonga soko la Omdurman wakati wa majibizano makali ya moto kati ya pande hizo mbili.
"Zaidi ya raia 20 wameuawa na wengine wamejeruhiwa," ilisema taarifa hiyo iliyotumwa kwa AFP. Kamati inafuatilia ukiukaji wa haki wakati wa vita na wahasiriwa wake wa kiraia.
Siku ya Jumamosi, chanzo cha matibabu kilisema makombora ambayo yalipiga nyumba huko Khartoum yaliwaua raia 15.
Idadi ya vifo inaongezeka
Omdurman mara kwa mara imekuwa eneo la vita vikali kati ya pande hizo mbili.
Ingawa mapigano mengi hapo awali yalizuiliwa katika mji mkuu na eneo la magharibi la Darfur, pia yameenea hadi maeneo ya kusini mwa Khartoum kulingana na mashahidi.
Zaidi ya watu 10,000 wameuawa katika mzozo wa Sudan kufikia sasa, kulingana na makadirio ya kihafidhina ya mradi wa 'Armed Conflict Location & Event Data.'
Lakini makundi ya misaada na matabibu wameonya mara kwa mara idadi halisi inazidi idadi iliyorekodiwa, huku wengi wa waliojeruhiwa na kuuawa wakiwa hawafiki hospitalini au vyumba vya kuhifadhia maiti.
Vita hivyo vimesababisha takriban watu milioni 5.5 kukimbia, ndani ya Sudan na kuvuka mipaka, kulingana na Umoja wa Mataifa.