Rwanda imeishutumu Marekani kwa kumuwekea vikwazo Waziri wake wa nchi anayeshughulikia masuala ya kikanda James Kabarebe.
''Vikwazo kwa Waziri wa Nchi James Kabarebe havina msingi. Ikiwa vikwazo vingeweza kutatua mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), tungekuwa na amani katika eneo hilo miongo kadhaa iliyopita,” Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imesema katika taarifa.
Kwa miaka mitatu Rwanda imekuwa ikitaka kujuwa, kuhusu mzozo kwenye mpaka wa magharibi mwa Rwanda ambao umehusisha “vikosi vya uhasama” ilhali havijawekewa vikwazo.“ Hizi ni pamoja na vikosi vya jeshi la Congo (FARDC), mapigano pamoja na wanajeshi wa SAMIDRC, wanajeshi wa Burundi, wanamgambo wa mauaji ya halaiki wa FDLR, na mamluki kutoka Ulaya (ambao 300 kati yao hivi karibuni walisaidiwa na Rwanda kwenda salama hadi Romania),” imeongeza.
DRC, Umoja wa Mataifa na sasa nchi tofauti za kimataifa zinalaumu Rwanda kwa kuunga mkono kikundi cha waasi cha M23. Lakini Rwanda imeendelea kukana.Vikosi vya M23 vilianza mashambulizi tena Januari mwaka huu na vimeteka maeneo ya Mashariki na Kaskazini mwa DRC.
"Lengo pekee la Rwanda ni kuwa na mpaka salama, na kumalizwa kwa siasa za kikabila katika eneo letu. Hili ni suala la usalama wa taifa," Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imeongeza." Raia wa Rwanda wana haki ya kuishi kwa amani na bila kuwa na hofu au ukosefu wa usalama kutoka DRC," imesema.
Hii majuzi Ubalozi wa Rwanda nchini Uingereza umetoa tamko rasmi kufuatia kutakiwa kutoa maelezo na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, ikielezea kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama na hali tete ya mgogoro unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Ubalozi huo uliambia Uingereza kuwa Jeshi la Rwanda linachukua hatua za kujilinda kufuatia tishio la usalama.