Mamlaka ya usafiri wa anga ya Sudan imeongeza muda wa kufungwa kwa anga ya nchi hiyo hadi Agosti 15, isipokuwa kwa usaidizi wa kibinadamu na ndege za kuwahamisha, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum ulisema katika taarifa mapema Jumatatu.
Anga ya Sudan ilifungwa kwa usafiri wa kawaida punde baada ya mzozo wa kijeshi kuzuka kati ya jeshi la nchi hiyo na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katikati ya mwezi wa Aprili.
Vita kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani, kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, vimesababisha vifo vya takriban watu 3,900, kulingana na makadirio, na wengine milioni 3.5 wameyahama makazi yao. Wengi wa waliokimbia makazi yao walikimbilia nchi jirani.
Mapigano mengi yametokea katika vitongoji vilivyo na watu wengi vya Khartoum, na kusukuma wakaazi milioni 1.7 kukimbia na kuwalazimu mamilioni waliosalia kujikinga na milipuko ya moto katika nyumba zao, mgao wa maji na umeme.
Wakati huo huo, wanamgambo wa RSF wamewaamuru raia kuondoka majumbani mwao kusini mwa mji mkuu, wakaazi kadhaa walisema Jumapili, wakati mapigano kati ya vikosi vya majenerali wapinzani yakiendelea katika eneo la magharibi la Darfur.
"Wanachama wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) waliniambia nilikuwa na saa 24 kuondoka eneo hilo," mkazi wa Khartoum Fawzy Radwan aliambia AFP.
Milipuko ya mabomu inaendelea
Mamia ya wakaazi walikuwa wakifurushwa kutoka kitongoji cha Jabra kusini mwa Khartoum, kulingana na wakaazi siku ya Jumapili.
Jabra na eneo la karibu la Sahafa ni nyumbani kwa kikosi cha silaha za kijeshi pamoja na kituo cha RSF kinachotumiwa na Daglo.
"Walituambia hili ni eneo la kijeshi sasa na hawataki raia karibu," mkazi Nasser Hussein aliambia AFP. RSF imeshutumiwa kwa kukithiri kwa uporaji na kuwafurusha watu kwa nguvu kutoka kwa nyumba zao tangu vita kuanza Aprili 15.
Pamoja na Khartoum, baadhi ya ghasia mbaya zaidi zimekuwa katika eneo lenye migogoro la Darfur, ambako madai ya uhalifu wa kivita yameibua uchunguzi mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Tena siku ya Jumapili, mapigano katika mji wa Nyala - mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini na mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan -- yalipelekea mabomu kuangukia vitongoji vya kiraia, mashahidi walisema.
Katika mji mkuu wa jimbo la Darfur ya Kati Zalingei, jeshi "liliwaua waasi 16 na kuwakamata 14, akiwemo afisa mmoja", chanzo cha kijeshi kiliiambia AFP siku ya Jumapili, kikiomba kutotajwa jina kwa vile hawakuwa na idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari.