Majeruhi wa mlipuko wa gesi uliotokea jijini Nairobi wanapigania maisha yao huku serikali ikisema tayari watu wawili wamepoteza maisha.
"Serikali ya Kenya imethibitisha kwamba jana Alhamisi tarehe 1 Februari 2024, mwendo wa saa tano na nusu jioni, kulitokea mlipuko mkubwa katika eneo la Embakasi, Kaunti ya Nairobi," Dk. Isaac Mwaura msemaji wa serikali amesema katika taarifa.
"Lori moja lenye namba ya usajili ambayo haijajulikana lililokuwa limesheheni gesi lililipuka na kusababisha moto mkubwa uliosambaa," Mwaura ameongezea.
Mtungi wa gesi ulioruka uligonga sehemu ya kuhifadhi mizigo ya kampuni inayoitwa Oriental na kuwasha moto katika eneo hilo lenye nguo.
Msemaji wa serikali amesema moto huo mkubwa umeharibu zaidi magari kadhaa na mali, pamoja na biashara nyingi ndogo na za kati.
"Cha kusikitisha ni kwamba nyumba za makazi katika kitongoji hicho nazo ziliteketea kwa moto, huku idadi kubwa ya wakazi wakiwa bado ndani kwani ilikuwa ni usiku sana. Kutokana na hali hiyo. Wakenya wawili wamepoteza maisha," Mwaura ameongezea.
Aidha, Wakenya wengine 222 walijeruhiwa na moto huo, na wamekimbizwa katika hospitali mbalimbali.
Serikali imetoa tahadhari kwa wananchi kuepuka eneo hilo ili kuruhusu shughuli ya uokoaji kutekelezwa bila usumbufu.