Fighting in Khartoum

Bei za juu za bidhaa, ukosefu wa hospitali na hata maeneo ya kuzika maiti ni moingoni mwa vilio vya wakaazi wa Sudan wanao endelea kuhimili dhoruba za mabomu na milio ya risasi ya kila siku.

Kufungwa kwa hospitali na mashambulizi dhidi ya vituo vya kutolea huduma za afya na pande mbili zinazozozana tayari kumesababisha uhaba wa dawa na matatizo kwa wagonjwa, hasa wale walio na magonjwa sugu, kulingana na vyanzo vya mamlaka ya afya nchini humo.

"Zaidi ya hospitali 40 kati ya 57 mjini Khartoum bado zimefungwa, na hii imekuwa na athari mbaya sana kwa mfumo wa afya ambao tayari ulikuwa na mapungufu makubwa kabla ya vita kuanza," waliiambia shirika la habari la Anadolu, kwa sharti la kutotajwa jina kwa sababu za kiusalama.

Bei za vyakula na bidhaa nyingine zimepanda kwa kasi katika maeneo yanayodhibitiwa na Wanajeshi wa Sudan nje ya Khartoum, kutokana na ukosefu wa usambazaji na uhaba wa mafuta, umeme, maji na mahitaji mengine.

"Ingawa tunaishi katika kitongoji salama zaidi cha Althawra katika jiji la Omdurman, hatuwezi kutoka nje ya nyumba zetu kutafuta mahitaji ya kimsingi tunayohitaji," Hussien Mohamed wa eneo hilo aliiambia Anadolu.

"Wengi wa majirani zetu wamehama makazi yao, na hali inatisha sana. Wafanyabiashara nao ni 'walafi' kwa kuongeza bei kwa sababu wanataka kutumia mahitaji ya watu na ukosefu wa ufuatiliaji wa serikali," Mohamed alisema.

Umoja wa Mataifa ulionya kwamba nusu ya wakazi wa Sudan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na wako kwenye hatari ya kukumbwa na njaa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la chakula duniani FAO, ''watu milioni 20.3, sawa na asilimia 42 ya idadi ya watu nchini humo wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula kati ya Julai na Septemba 2023.'' ripoti hiyo ilisem.

Taarifa kutooka ndanxi ya Sudan pia zinasema kuwa wakaazi wameshindwa kumudu mazishi ya wapendwa wao kutokana na mapigano hayo.

Abdallah Alhassan alilazimika kumzika kaka yake katika ua la nyumbani kwao eneo la Omdurman mwezi Agosti kwa sababu familia haikuweza kuupeleka mwili wake kwenye makaburi ya karibu.

“Ndugu yangu aliuawa baada ya bomu kulipuka nyumbani kwetu wiki iliyopita tukiwa tumelala, tulijaribu na baadhi ya majirani zetu kumzika makaburini, lakini mapigano ya siku hiyo Omdurman yalikuwa makali sana, hivyo tuliamua kumzika ndani ya nyumba, na tukaondoka nyumbani kwenda kukaa na jamaa zetu huko Atbara," aliambia Anadolu.

Hakuna mtu nchini Sudan aliyetarajia vita vilivyozuka kati ya jeshi na kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) vingedumu kwa karibu miezi mitano bila dalili ya wazi ya kupatikana suluhu.

Hakuna kusitisha mapigano au kufunguliwa kwa njia za kupitisha misaada ya kibinadamu.

AA