Akiongea katika mkutano wa waandishi wa habari wa pamoja Ankara, Rais wa Uturuki Erdogan amemshukuru Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu wa Ethiopian Abiy Ahmed kwa "mapatano ya kihistoria". / Picha: AA

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amempongeza Rais wa Somali na Waziri Mkuu wa Ethiopia kwa kufikia "makubaliano ya kihistoria na kujitolea kwa hali ya juu" katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika Ankara ambayo yanalengo la kumaliza mgogoro wa eneo lililojitenga la Somaliland.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Ankara siku ya Alhamisi, Erdogan amemshukuru Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kutangaza kwamba pande zote mbili zimekubaliana katika tangazo la pamoja kutatua mgogoro ulioko.

"Tumechukua hatua ya kwanza kuelekea mwanzo mpya uliojikita katika amani, mashirikiano kati ya Somalia na Ethiopia," amesema Erdogan.

Tegemeo kubwa la Ankara ni kuleta amani na utulivu, "katika eneo hilo muhimu" la Afrika kati ya Somalia na Ethiopia, ameongeza.

Uturuki inaamini makubaliano kati ya Somalia na Ethiopia yataweka msingi madhubuti wa mashirikiano na maendeleo yaliyojikita katika misingi ya kuheshimiana, ameongeza.

Rais wa Somalia Mohamud amepongeza jitihada za Uturuki katika kutatua migogoro ya kikanda na kisiasa kati ya Somalia na Ethiopia, na kuongeza kuwa nchi yake daima imekuwa ikitaka kuwa "rafiki wa kweli na Ethiopia."

Waziri Mkuu wa Ethiopia Ahmed pia alipongeza jitihada za Uturuki na kuyaita makubaliano yaliyofikiwa Ankara kama "mazungumzo ya kifamilia" ambayo yalileta ushindi kwa nchi yake na nchi jirani ya Somalia.

Kwa mujibu wa Tangazo a Ankara, pande zote mbili zimeamua kuanzisha majadiliano, huku Uturuki ikiwezesha, kufikia mwishoni mwa mwezi Februari, 2025 na kuyamaliza katika kipindi cha miezi minne.

Pande zote mbili zimehakikisha kuheshimu mipaka ya Somalia huku ikitambua uwezekano wa Ethiopia wa kunufaika na ufikiaji wa bahari.

Hali ya wasiwasi kati ya Ethiopia-Somalia

Uhusiano kati ya Ethiopia na Somalia ulikuwa mbaya baada ya makubaliano ya Januari 1 kati ya Ethiopia na eneo lililojitenga la Somaliland kutumia bandari ya Berbera.

Uturuki imekuwa ikifanya kazi kumaliza mvutano kati ya nchi hizo mbili.

Ethiopia ilipoteza bandari yake ya Bahari Nyekundu mwanzoni mwa miaka ya 90 baada ya vita vya uhuru wa Eritrea, vilivyoisha 1991.

Mwaka 1991, Eritrea ilipata uhuru kutoka Ethiopia, na kupelekea kuundwa kwa mataifa mawili. Hali hiyo ilipelekea Ethiopia kupoteza ufikaji wa moja kwa moja wa eneo la Bahari Nyekundu na bandari muhimu.

Tangu wakati huo, Ethiopia imekosa bahari na kuathiri uwezo wake wa kufanya shughuli za baharini.

TRT World