ECOWAS yatuma ujumbe wa kidiplomasia nchini Senegal kuhusu uchaguzi ulioahirishwa

ECOWAS yatuma ujumbe wa kidiplomasia nchini Senegal kuhusu uchaguzi ulioahirishwa

Spika wa bunge la Ecowas amepanga kukutana na mamlaka ya Senegal, wanasiasa na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.
Maandamano yamefanyika kote nchini kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais. / Picha: Reuters

Jumuiya kuu ya kiuchumi na kisiasa ya Afrika Magharibi ECOWAS imetuma ujumbe wa kidiplomasia nchini Senegal kujadili hali ya kisiasa huko kufuatia kucheleweshwa kwa uchaguzi wake wa rais, ofisi ya bunge ya umoja huo ilisema Jumatatu.

Wakati wa misheni hiyo ya siku mbili spika wa bunge la ECOWAS, Sidie Mohamed Tunis, na wajumbe wa bunge hilo watakutana na mamlaka ya Senegal, wanasiasa na wawakilishi wa mashirika ya kiraia, ilisema katika taarifa.

Ujumbe huo ulipangwa kuwasili Senegal siku ya Jumatatu.

Watu watatu wameuawa katika makabiliano ya wiki iliyopita kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama kuhusu kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

Mwanafunzi auawa

Maandamano makali yalizuka kote nchini Ijumaa iliyopita, yakiongozwa na vyama vya siasa vya upinzani na baadhi ya mashirika ya kiraia yanayopinga kucheleweshwa kwa uchaguzi.

Wahasiriwa ni pamoja na mwanafunzi wa shule ya upili mwenye umri wa miaka 19, muuza duka Modou Gueye mwenye umri wa miaka 23 na mwanafunzi wa chuo kikuu, tovuti ya habari ya Seneweb iliripoti, ikinukuu vyanzo vya hospitali.

Waziri wa mambo ya ndani Sidiki Kaba amekanusha ripoti za vyombo vya habari kuwa vikosi vya usalama vilihusika na kifo hicho.

Umoja wa Ulaya Jumapili ulitoa wito kwa mamlaka ya Senegal kudhamini "uhuru wa kimsingi" huku kukiwa na maandamano.

Mapema mwezi huu 3, Rais wa Senegal Macky Sall alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa rais, akitaja mzozo kuhusu orodha ya wagombea na madai ya ufisadi wa majaji wa kikatiba.

Bunge la Kitaifa la Senegal wiki iliyopita liliunga mkono mswada wa kuahirisha uchaguzi wa rais wa Februari 25 hadi Desemba 15, wakati wa kikao cha mvutano ambapo wabunge wa upinzani waliondolewa kwa nguvu kwenye ukumbi huo.

Baraza la Katiba linatarajiwa kutoa uamuzi katika takriban wiki moja kuhusu suala hilo.

TRT Afrika