Gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini, Jenerali Constant Ndima alishutumu kitendo cha waasi wa M23 kuteka baadhi ya maeneo ambayo walisha furushwa kwenye wilaya za Rutshuru, Masisi na Nyiragongo licha ya kupelekwa kwa wanajeshi wa EAC.
Afisa mkuu wa askari jeshi wa Congo alizungumza katika mkutano wa pamoja na kamanda wa jeshi la kanda ya EAC.
Wakazi kadhaa wa eneo hilo wanaiambia TRT Afrika kua wanataka wanajeshi wa EAC ambao tayari wako Kongo kuweka shinikizo kubwa kwa waasi wa M23 ili mgogoro huu umalizike haraka iwezekanavyo badala ya kuendelea kuongeza vikosi vipya kila uchwao.
''Tayari tunao wajeshi ya Umoja wa mataifa, ambao wamekuwa nchini kwa zaidi ya miaka 20, na bado hatuja pata suluhisho kwenye mgogoro wa DRC. Kwa nini tena waongeze wengine majeshi?'' anashangaa Mumbere Muyisa, mkazi wa Goma akihojiwa na TRT Afrika kwa njia ya simu.
Kwa upande wake, kamanda wa kikosi cha kanda cha EAC, Jenerali Jeff Nyagah asisitiza kujitoa kwa askari wa EAC chini ya uongozi wake, kusaidia na kulinda uadilifu wa eneo la DRC.
Wakati wa mkutano na mawaziri Ijumaa iliyopita, serikali ya Kongo ilitangaza kwamba waasi wa M23 wanaimarisha kambi zao katika maeneo ya Rutshuru, Masisi na Nyiragongo.
Lawrence Kanyuka, msemaji wa kisiasa wa M23 alisema kwamba kama hakuna Mazungumzo ya Kisiasa ya Moja kwa Moja kati ya M23 na Serikali ya Kinshasa, pia hakutakuwa na utatuzi, upokonyaji silaha na uondoaji jeshi.
Hata hivyo hitaji lao bado ni ndoto kwani Rais Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo alisisitiza kwa mara nyingine tena kwamba hakuna suala la mazungumzo yoyote ya kisiasa na waasi wa M23.