Mfululizo wa mabomu walipua na kuharibu majumb ya makaazi eneo la Gaza, Jumapili, / Picha:: AFP

Jumatatu, Oktoba 9, 2023

0748 GMT - Hamas inataka "kuwakomboa wafungwa wote wa Kipalestina" kutoka Israel na kukomesha chokochoko za Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Jerusalem, hasa katika Msikiti wa Al Aqsa, msemaji wa kundi hilo Abdel Latif al Qanoua amesema.

"Tuko kwenye vita vya wazi vya kutetea watu wetu na Msikiti wa Al Aqsa," alisema. "Vita hivi vinahusishwa na ukombozi wa wafungwa wote wa Kipalestina na kusitishwa kwa shughuli za serikali hii ya kifashisti huko Jerusalem."

Alisema kundi hilo limekamata "idadi kubwa ya Waisraeli" huko Gaza, bila kutoa takwimu maalum. Alisema tawi la kijeshi la Hamas, al Qassam, litatangaza takwimu hizo baadaye.

0529 GMT - Jeshi la Israeli bado linapambana na Hamas

Mapigano kati ya vikosi vya Israel na wapiganaji wa Hamas yanaendelea katika maeneo saba hadi nane karibu na Gaza, jeshi lilisema.

"Bado tunapigana. Kuna kati ya maeneo saba hadi nane ya wazi karibu na Gaza (ambapo) bado tuna wapiganaji wanaopigana na magaidi," msemaji wa kijeshi Richard Hecht aliwaambia waandishi wa habari, siku mbili baada ya kundi la Palestina kufanya mashambulizi ya kushtukiza katika miji ya Israel karibu na Gaza. .

0207 GMT - Umoja wa Mataifa unasema idadi ya wakazi wa Gaza waliokimbia makazi yao imeongezeka hadi zaidi ya 123,000 kutokana na mapigano kati ya jeshi la Israel na Hamas kufuatia mashambulizi ya kundi hilo dhidi ya Israel ambayo hayajawahi kushuhudiwa.

Kufikia Jumapili, mashambulio ya ndege ya kulipiza kisasi ya Israeli yalikuwa yameharibu nyumba 159 kote Gaza na kuharibu vibaya nyingine 1,210, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina limesema shule inayohifadhi zaidi ya watu 225 ilipata pigo moja kwa moja.

Vyombo kadhaa vya habari vya Israel, vikiwanukuu maafisa wa huduma ya uokoaji, vilisema takriban watu 700 wameuawa nchini Israel.

Wizara ya Afya ya Gaza imesema watu 413 wakiwemo watoto 78 na wanawake 41 waliuawa katika eneo hilo.

Takriban watu 2,000 wamejeruhiwa kila upande.

0201 GMT - Palestina: Msaada wa kimataifa kwa Israeli unahimiza uhalifu zaidi

Waziri Mkuu wa Palestina Mohammad Shtayyeh alisema Jumapili kwamba uungaji mkono wa kimataifa kwa Israel unaihimiza kufanya uhalifu zaidi.

Katika taarifa yake, Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Wizara Kuu ya Palestina ilisema kuwa Shtayyeh alipiga simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly kuhusu matukio ya hivi punde huko Palestina na Israel.

Shtayyeh alisema kuwa "jukumu lote" kwa kile kinachotokea ni la Israeli, ambayo imeunda "mazingira ya chuki, vurugu na uchochezi na kukiuka sheria za kimataifa."

0104 GMT - Takriban Wapalestina sita waliuawa na moto wa Israel katika Ukingo wa Magharibi

Takriban Wapalestina sita waliuawa katika mapigano na wanajeshi wa Israel katika miji kadhaa ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Katika msururu wa taarifa, Wizara ya Afya ya Palestina ilisema kuwa mtu mmoja aliuawa huko Jeriko, watatu huko Qalandia kaskazini mwa Jerusalem na mmoja huko Al-Khalil na Nablus kwa risasi na vikosi vya uvamizi.

Wizara hiyo ilisema miili ya vijana hao watatu kutoka Qalandia imehamishiwa katika kituo cha matibabu huko Ramallah.

Shirika rasmi la habari la Palestina WAFA limeripoti kuwa vikosi vya Israel vimewafyatulia risasi za moto vijana hao watatu katika makabiliano kwenye kizuizi cha kijeshi.

TRT Afrika