Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana Jumanne / picha ya UN

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana Jumanne kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kwa ajili ya mjadala wao wa wazi uliopangwa wa kila robo ya mwaka.

Hii ni mara ya nne kwa mabalozi 15 wa Baraza Kuu la Amani na Usalama la Umoja wa Mataifa kukutana tangu mzozo kati ya Israel na Palestina kuanza tarehe 7 Oktoba.

Hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota huku mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yakiendelea.

" Ni lazima tudai kwamba pande zote zitekeleze na kuheshimu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres aliwaambia wajumbe wa mkutano.

"Ni muhimu kuchukua tahadhari mara kwa mara katika uendeshaji wa operesheni za kijeshi ili kuwaokoa raia na kuheshimu na kulinda hospitali na kuheshimu vituo vya Umoja wa Mataifa ambavyo leo vinahifadhi zaidi ya Wapalestina 600,000," Gutteres aliongezea.

Israel yamtaka Katibu Mkuu wa UN kujiuzulu

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan alitoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa "kujiuzulu moja."

Kuna nchi ambazo zimesema lazima Israel isitishe mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina / Picha: Reuters 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Eli Cohen pia aliandika katika tweet yake kwamba hatakutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mazungumzo yaliyopangwa kufanyika.

“Tunaenda kushinda kwa sababu vita hivi ni vya maisha, vita hivi lazima viwe vita yako pia,” alisema na kuongeza, "Hivi sasa, ulimwengu unakabiliwa na chaguo la uwazi wa maadili."

Balozi Erdan alikashifu tamko la Gutteres kuwa "mashambulizi ya Hamas hayakuibuka bure."

Aliwaambia waandishi wa habari katika kikao hicho kwamba kwa kutambua mashambulizi ya Hamas "hayakutokea bure" katika hotuba yake ya Baraza, Gutteres "anahalalisha ugaidi."

Misimamo tofauti

Mjadala huo wa Baraza la Usalama lilipata maoni tofauti kutoka kwa wajumbe wa nchi tofauti.

Riyad al-Maliki ambae ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Palestina alisema kuwa Baraza la Usalama na Jamii ya kimataifa lina wajibu wa kuokoa maisha. "Baraza hili la Usalama halina sababu ya kuendelea kushindwa," alisisitiza.

Zaidi ya Wapalestina milioni moja wameripotiwa kuwa wamekimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya Israel huko Gaza Picha: AFP

Sameh Shoukry, waziri wa mambo ya nje wa Misri alisema maeneo ya Palestina yanapitia matukio ya kutisha, akibainisha kuwa maelfu ya watu wameuawa huko, ikiwa ni pamoja na maelfu ya watoto. "Ni aibu kwamba wengine wanaendelea kuhalalisha kile kinachotokea, wakitaja haki ya kujilinda na kupinga ugaidi."

Mwakilishi wa Syria Al Haka Dindi, alisema kampeni ya jinai na umwagaji damu ya Israel ilikuwa zaidi ya ufahamu na mawazo.

"Kampeni hii haramu isingewezekana kama baadhi ya Mataifa ya Magharibi yasingetoa ukweli kwa kile wanachoeleza kuwa ni haki ya kujilinda." aliiambia mkutano.

Balozi Alya Ahmed Seif Al-Thani wa Qatar, akijihusisha na Kundi la Waarabu, aliliambia Barala la Usalama kuwa zaidi ya wiki mbili zilizopita, limetoa wito na juhudi za kidiplomasia bila kuchoka kwa upatanishi na mazungumzo kuelekea utatuzi wa amani wa mzozo huo.

Mkurugenzi mkuu wa UN amesema hali inazidi kuzorota huko Gaza / Picha: AFP

Alisema Qatar inakashifu vikali maneno ya Israel ambayo yalitoa taswira potofu ya juhudi za upatanishi za nchi yake.

Annalena Baerbock, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, alisema nchi yake inaendelea kusimama na Israel.

"Usalama wa Israeli hauwezi kujadiliwa. Kama nchi nyingine yoyote ulimwenguni, Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya ugaidi ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa." alisema.

Vasily Nebenzya balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa alisisitiza msimamo wa Urusi kwamba kunahitajika mchakato endelevu wa mazungumzo.

"Mgogoro huu umeonyesha tena kwamba bila ya kusuluhishwa kwa haki mzozo wa Palestina na Israel kwa kuzingatia maazimio ya Baraza la Usalama na Baraza Kuu na kwa kuzingatia maamuzi yaliyoidhinishwa ya kimataifa juu ya suluhisho la mataifa mawili , utulivu wa kikanda hautaweza kufikiwa," aliongeza.

Baraza la Amani na Usalama la UN lilishindwa kupitisha rasimu ya maazimio mawili ya awali kuhusu ongezeko hilo.

Wa kwanza kutoka Urusi ikitaka kusitishwa kwa mapigano mara moja, ilishindwa kupata kura za kutosha.

Rasimu ya Brazil ilipigiwa kura ya turufu na Marekani.

Ingawa ilitaka kusitishwa kwa vita kwa muda kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kuingizwa Gaza, Marekani iliipinga kwa madai kuwa haikutaja haki ya Israeli ya kujilinda.

Mashambulio ya mara kwa mara ya Gaza na vikosi vya Israeli, kiwango cha vifo vya raia, na uharibifu wa jumla wa vitongoji unaendelea kuongezeka na ni ya kutisha sana.

TRT Afrika